HUU ni mwaka
wa neema Simba SC. Huu ndio ukweli kwani baada ya kukubali kubadili mfumo wa
uendeshaji wa klabu hiyo ambao utaruhusu bilionea, Mohamed Dewji maarufu kama
Mo kuwekeza fedha nyingi, klabu hiyo sasa iko mbioni kupata dili lenye pesa
nyingi za udhamini.
Katika mfumo
mpya, Mo atawekeza kiasi cha Sh bilioni 20 kwa kununua hisa 51 za klabu hiyo
huku hisa nyingine zikinunuliwa na wadau wengine wakiwemo wanachama wa klabu
hiyo kongwe ya jijini Dar es Salaam.
Mbali na
uwekezaji huo, klabu hiyo sasa ipo katika hatua za mwisho za mazungumzo ya
udhamini na Benki ya NMB hasa baada ya kumalizika kwa mkataba wa udhamini na
Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) ambayo ilikuwa ikiidhamini klabu hiyo kupitia bia
yake ya Kilimanjaro.
Mwenyekiti
wa Kamati ya usajili ya klabu hiyo, Zacharia Hanspope, aliliambia BINGWA kuwa
klabu hiyo ipo kwenye mipango kabambe ya kupata wadhamini mbalimbali ili
kuhakikisha wanatunisha mfuko wa klabu hiyo na moja ya wadhamini hao ni NMB.
“Mpaka sasa
NMB ndio wameonyesha nia ya kutudhamini, mazungumzo yako katika hatua nzuri
sana lakini pia bado milango iko wazi kwa ajili ya makampuni na mashirika
mengine,” alisema.
Hata hivyo,
Hanspope alikataa kuweka wazi thamani ya mkataba huo, lakini alisema kwamba
utakuwa ni moja ya mikataba minono itayoinufaisha Simba na kuipa fedha za
uhakika kulingana na thamani na ukubwa wa klabu hiyo.
NMB ambayo
inaidhamini Azam kwa miaka miwili ambapo klabu hiyo ya Chamazi jijini Dar es
Salaam, imenufaika kutokana na udhamini huo ambao kila mwaka ilielezwa walipata
milioni 500 kutokana na udhamini huo.
Azam ilikuwa
ikivaa jezi zenye nembo ya NMB kifuani kuanzia mazoezini hadi kwenye mechi zote
walizokuwa wanashiriki za Ligi Kuu na zile za mashindano ya kimataifa.
Awali Simba
iliwahi kuingia mkataba na benki hiyo mwaka 2004, lakini baadaye mkataba huo
ulivunjika kabla ya kumalizika kutokana na kukiukwa kwa makubaliano ya mkataba
huo.
Pia NMB
iliwahi kuidhamini timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars kati ya mwaka 2007 na
2010 ikiwa chini ya kocha Mbrazil, Marcio Maximo.
Post a Comment