KOCHA Mkuu wa Simba, Mcameroon, Joseph Omog, amebadili mbinu
za ufungaji mabao huku akiwatumia mawinga na mabeki wake wa pembeni kuanzisha
mashambulizi.
Hiyo ni siku chache tangu timu hiyo itoke suluhu na JKT Ruvu
kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa wikiendi iliyopita katika Uwanja wa
Taifa jijini Dar es Salaam.
Safu ya mawinga ya timu hiyo inaundwa na Shiza Kichuya na
Jamal Mnyate huku mabeki wa pembeni wakiwa ni Mohammed Hussein Zimbwe na Malika
Ndeule.
Omog alisema amepanga
kutumia mipira ya pembeni katika kuanzisha mashambulizi baada ya mechi ya JKT
Ruvu kupata ugumu wa kupenyeza mipira katikati kutokana na uimara wa safu ya
ulinzi ya wapinzani wake.
Omog alisema, anaamini hiyo ni njia sahihi kwake katika
upatikanaji wa mabao mara watakapokutana na timu inayocheza kwa kulinda lango
lao wakati wote kwa kujazana wachezaji wengi nje ya 18.
Mcameroon huyo alisema, mechi ya JKT Ruvu walipata ugumu wa
kufunga kutokana na wapinzani wao kucheza soka la kujilinda muda wote kwa
kujazana langoni mwao.
Aliongeza kuwa, tayari ameanza kuwandaa mawinga na mabeki
wake wa pembeni kwa kuwapa mbinu mbalimbali za jinsi ya kushambulia kwa kupiga
krosi safi zitakazofika kwa washambuliaji wake wenye maumbile makubwa, Laudit
Mavugo na Frederick Blagnon kwa ajili ya kufunga kwa kupiga vichwa.
"Kama ulivyoona katika programu ya mazoezi ya mwisho
tuliyoyafanya kwenye Uwanja wa Boko Veterani siku moja kabla ya mechi hii ya
JKT Ruvu, uliona jinsi nilivyokuwa nikiwaelekeza mabeki wa pembeni na mawinga
wangu wanavyotakiwa kupiga krosi na kona zitakazowafikia washambuliaji wangu
huku nikiwataka kufunga kwa kichwa.
“Kikubwa ninataka kuona tunatafuta mbinu nyingine mbadala za
kufunga mabao kwa kutokea pembeni kwa mabeki na mawinga kupiga krosi hizo nzuri
na siyo kulazimisha kufunga kwa kupenya katikati.
“Mfano uliona mechi na JKT Ruvu walijazana mabeki wengi
katikati na kusababisha tushindwe kupenya kwa kupenyeza mipira kwa
washambuliaji kutokana na rundo la mabeki, hivyo nimejaribu mbinu hiyo nyingine
ya kutafuta mabao kwenye goli la timu pinzani, nafikiri nitaitumia kwenye
michezo kadhaa ijayo nione kama ina mafanikio,” alisema Omog.
Post a Comment