WAKATI uongozi wa Klabu ya
Simba ukitarajia kumfanyia uchunguzi zaidi beki wake, Hamad Juma ambaye alipasuka
kichwani sehemu ya kisogoni kutokana na kuanguka bafuni, kuna lingine limeibuka
jipya.
Hamad alipata jeraha hilo
baada ya kuanguka bafuni na kuvuja damu nyingi hali iliyofanya akimbizwe Hospitali
ya Mwananyamala jijini Dar, alipotoka alipewa wiki moja ya mapumziko ambapo
aliamua kwenda nyumbani kwao kwa matibabu zaidi.
Lakini mara baada ya kutua
Tanga juzi kufuatia kupewa ruhusa, uongozi umeshindwa kumpata kwa kuwa namba ya
simu anayotumia haipatikani na mpaka kufikia jana jioni hawakuwa na taarifa
zake zozote juu ya maendeleo yake.
Championi Ijumaa
lilipowasiliana na mchezaji huyo kupitia simu yake ya mkononi halikuweza
kumpata, alipopigiwa simu Meneja wa Simba, Mussa Mgosi naye alikiri kuwa
hawajampata hewani mchezaji huyo.
“Tangu alipoondoka hatujampata
hewani, nimempigia katika namba yake ninayoifahamu sijampata, lakini nitauliza
kwa wachezaji wenzake kama kuna namba nyingine ambayo anatumia ili nijue
maendeleo yake, si unajua tulimpa muda wa wiki moja kupumzika kama
tulivyoshauriwa na madaktari? Hivyo nikipata taarifa zaidi nitakujulisha.”
Hamad alikutwa na tukio hilo siku
moja tu baada ya mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ndanda FC, ambapo
alilazwa kwa siku moja hospitalini.
Mgosi aliongeza pia kuwa mpaka
anaondoka kwenda Tanga, alikuwa anaendelea vizuri na kurejea uwanjani
itategemea na ripoti ya daktari.
Akimzungumzia mchezaji huyo, Daktari
wa Simba, Yassin Gembe, aliliambia gazeti hili kuwa maendeleo yake ni mazuri na
wanaamini baada ya wiki mbili atakuwa fiti kuanza mazoezi mepesi kwa ajili ya
kujiweka sawa.
“Tumetoa
muda huo kwa sababu hakupata matatizo makubwa kwenye ubongo pamoja na baadhi ya
mifupa yake ya kichwani zaidi ya ile kupasuka pekee na kupoteza damu jambo ambalo
kitaalamu halina athari sana na mara baada ya muda huo tuliompa atakuwa sawa,” alisema
Gembe.
Post a Comment