MSHAMBULIAJI
wa Simba raia wa Ivory Coast, Fredrick Blagnon,
ameanza kuzua hofu kwa mahasimu wa jadi wa klabu hiyo, Yanga, baada ya
kuonyesha uwezo wa hali ya juu katika mechi alizocheza Uwanja wa Taifa, ikiwemo
mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Ndanda.
Simba
walishinda mabao 3-1, huku Blagnon akifunga bao la pili kwa kichwa na kuanza
kuzamisha jahazi la Ndanda ambao walikuwa na matumaini ya kuibuka na sare
kwenye mchezo huo.
Blagon,
aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Ibrahim Ajib, alibadilisha sura
ya mchezo huo kwa Simba ambayo ilipanga vyema mashambulizi yake na hatimaye
kupata bao la pili na la tatu.
Kutokana na
uwezo ulioonyeshwa na Blagon, watani wao wa jadi, Yanga, wameanza kutishika
huku uwezo wa mchezaji huyo ukiibua mjadala mkubwa kwa mashabiki wa Yanga
kuelekea katika mchezo wao wa ligi Oktoba mosi, mwaka huu.
Habari
zilizopatikana jana zilieleza kwamba benchi la ufundi la Yanga, linaloongozwa
na Hans van der Pluijm, limeanza kukuna kichwa jinsi ya kukabiliana na
washambuliaji wa Simba, akiwemo Blagon, ambaye ameonekana kuwa na uwezo mzuri.
Benchi la
ufundi la Yanga sasa linajipanga pamoja na mambo mengine, kuhakikisha viungo
wao, Thaban Kamusoko na Haruna Niyonzima wanakuwa na mbinu za kukabiliana na
Blagon, ambaye licha ya kwamba anacheza nafasi ya ushambuliaji, lakini
ameonekana kuwa ni mtu anayeweza kusumbua pia nafasi ya kiungo.
Katika hatua
nyingine, Katibu Mkuu wa Simba, Patrick
Kahemele, amesema Blagnon atawakimbiza mabeki na viongo wa timu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania
Bara kutokana na uwezo wake uwanjani.
Kahemele
alisema Blagnon msimu huu anaweza kuwa mfungaji bora kutokana na uwezo mkubwa
wa kupachika mabao kwa kutumia kichwa na miguu.
“Huyu jamaa
ni hatari sana, subiri uje uone wapinzani watakavyolizwa na mabao yake, tena
nakwambia atakuwa mfungaji bora msimu huu, kutokana ana kila sifa ya kuwa
mshambuliaji,” alisema Kahemele.
Blagon,
pamoja na kwamba atatumika kama mshambuliaji, lakini yeye ni kiungo
mchezeshaji, hivyo Kocha wa Simba, Joseph Omog, anaweza kumtumia katika nafasi
yoyote kati ya hizo na katika mechi ngumu kama ya Yanga huenda akamtumia katika
nafasi ya kiungo.
Post a Comment