KOCHA Mkuu wa Simba, Joseph Omog, ameanza kutengeneza kombinesheni hatari katika safu yake ya ushambuliaji kwa kuwatumia pamoja mastraika wake wawili wa kimataifa Mrundi, Laudit Mavugo na Muivory Coast, Frederic Blagnon.

Katika mazoezi ya jana ya Simba yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Boko Veterani jijini Dar es Salaam, kuanzia saa 9:00 alasiri, Omog alionekana akiwatumia Mavugo na Blagnon kama washambuliaji pacha wakati akiwapika kucheka na nyavu.

Mavugo na Blagnon ambao walionekana kuelewana vizuri, walitakiwa kumalizia  mashambulizi ambayo yalikuwa yanakitokea pembeni na kwenye eneo la kiungo na kutikisa nyavu kwa staili mbalimbali.

Kwenye mazoezi hayo, wachezaji wa Simba kila mmoja alitaka kuonyesha ubora wake kwa kocha Omog ili kujihakikishia namba kwenye kikosi cha kwanza, kitu ambacho kilisababisha upinzani mkali  katika mechi ya mazoezi iliyokuwa ikichezwa kati ya wachezaji wa kikosi cha kwanza na cha pili.

Katika hatua nyingine, Omog alisema  mazoezi yake sasa yamelenga zaidi kuwapika mastraika wake kucheka na nyavu, ili timu yake iwe moto wa kuotea mbali kwenye msimu huu wa Ligi Kuu ya Vodacoma Tanzania Bara.

“Tutafanya mazoezi kwa mafungu mawili leo mchana (jana), kwanza nitaanza kuwapika washambuliaji wangu peke yao, kabla ya kuongoza mazoezi ya kikosi kizima,” alisema Omog.

Post a Comment

 
Top