KATIKA hali ya kushangaza, wachezaji wa Yanga,
juzi Jumamosi waligoma kufanya mazoezi ya mwisho kabla ya kusafiri kuelekea DR
Congo kwa ajili ya mchezo wao wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya TP Mazembe
yaliyokuwa yakiongozwa na kocha mkuu wa timu hiyo, Mholanzi, Hans van Der
Pluijm kutokana na madai ya Sh milioni 100 wanazodai zikiwemo za usajili.
Yanga, Ijumaa iliyopita ilifanya mazoezi katika
Uwanja wa Uhuru kabla ya juzi Jumamosi kugoma kabisa kuendelea na programu hiyo
kufuatia madai hayo wakiushinikiza uongozi uwalipe fedha zao ambazo uliwaahidi
hapo awali kutokana na kufanya vizuri msimu uliopita.
Championi ambalo Jumamosi lilifika uwanjani hapo,
liliwashuhudia wachezaji hao wakiwa wamekaa na nguo zao za nyumbani tofauti na
ilivyozoeleka kabla ya kuamua kutoka uwanjani na kila mmoja kuchukua njia yake
huku Pluijm akiendelea kupanga vifaa vya kufanyia mazoezi siku hiyo zikiwemo
koni.
Wakati wachezaji wanafanya kikao chao, meneja wa
timu hiyo, Hafidh Saleh alikuwa na kikao kingine na kaimu katibu mkuu wa timu
hiyo, Baraka Deusdedit ambao nao kwa pamoja walianza kutoka ndani ya eneo la
uwanjani kuelekea kwenye basi la timu ikiwemo kutoa vifaa vyote na kuanza kuviweka
ndani ya basi huku Pluijm naye akiamua kwenda kwenye gari lake kubadilisha nguo
kwa ajili ya kutoka uwanjani hapo.
Championi
lilimfuata meneja wa timu hiyo ambaye hakutaka kuongea chochote zaidi ya
kumtupia mpira Deusdedit ambaye alidai ndiye mwenye uwezo wa kuongea
kilichotea.
Hata hivyo, kiongozi huyo hakuwa tayari kulitolea
ufafanuzi jambo hilo zaidi ya kusikika akilalamika akisema: “Kiukweli hii timu
imeshanichosha yaani kila kitu ni shida, wanachama nao hivyohivyo na wachezaji
nao wamezua balaa lingine, sijui hata nifanye nini.”
Lakini taarifa za ndani zinasema kuwa wachezaji
hao wameamua kugoma wakishinikiza uongozi wa timu hiyo utekeleze ahadi
walizoahidiwa.
“Wachezaji
wameamua kugoma kwa sababu wanadai fedha nyingi kutoka kwa uongozi ambazo uliwaahidi
hapo awali zikiwemo fedha za kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara, ubingwa wa
Kombe la FA, kuwatoa APR katika Ligi ya Mabingwa Afrika na kufuzu hatua ya
makundi Kombe la Shirikisho Afrika.
“Fedha ni nyingi kwani zinafikia milioni 100
kutoka katika mashindano hayo yote, lakini wanaona hakuna kinachoeleweka, kila
siku yamekuwa maneno kwani pia wanadai na fedha za usajili wengi walikuwa
hawajamaliziwa, kitu ambacho kinawakatisha tamaa na morali ya kucheza, maana
hata ishu ya kuchukua ubingwa wa msimu huu sina hakika kama itawezekana,”
kilisema chanzo hicho.
Alipotafutwa kwa njia ya simu Makamu Mwenyekiti
wa Yanga, Clement Sanga, kwanza aliipokea vizuri, lakini mwandishi
alipojitambulisha, kiongozi huyo akakata simu na hata alipotumiwa ujumbe mfupi
wa maandishi hakujibu.
Katika hatua nyingine, kikosi cha Yanga jana
Jumapili kilisafiri kuelekea DR Congo kikiwa na wachezaji 19, watu saba wa
benchi la ufundi, kiongozi mmoja wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na kaimu
katibu mkuu wa klabu hiyo.
Timu hiyo imeenda nchini humo kumalizia mchezo wa
mwisho wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya TP Mazembe utakaopigwa kesho
Jumanne.
Post a Comment