KLABU ya Vital’O ya Burundi imeibuka na mpya baada ya kupanga kuja Dar es Salaam Septemba mwaka huu kwa ajili ya kudai fedha zao kiasi cha dola 5,000 za Kimarekani sawa na zaidi ya Sh milioni 13 za usajili wa straika wao wa zamani, Amissi Tambwe.
Tambwe alisajiliwa na Simba kutoka Vital’O mwaka 2013 na kucheza kwa mafanikio mpaka pale alipoachwa dakika za mwisho msimu wa 2014/15.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Burundi, Rais wa Vital’O, Benjamin Bekorimana, alisema wamekubaliana na Simba wakutane Septemba kwa ajili ya kumalizia ishu hiyo.

Alisema makubaliano na Simba waliojiwekea ni kumwachia Laudit Mavugo lakini pia wamalizane na ishu ya Tambwe.
“Sisi na Simba hatuna tatizo ni ndugu zetu na ndiyo maana tumemalizana na Mavugo, lakini tumekubaliana pia tumalizane ishu ya Tambwe,” alisema.
Licha ya kudaiwa fedha hizo, Simba walishaachana na Tambwe ambaye ni mfungaji bora msimu uliopita na sasa yupo kwa wapinzani wao wa jadi, Yanga.
CHANZO: BINGWA

Post a Comment

 
Top