IMEKUWA ni kama kawaida sasa
lakini ni jambo la kustaajabisha kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutoa
taarifa zisizokuwa sahihi kwenye akaunti yake ya Mtandao wa Kijamii wa Twitter.
Siku za nyuma TFF kupitia
akaunti yake hiyo iliwahi kuandika tofauti baadhi ya matokeo ya mechi hasa
ilipocheza timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kwenye kuwania kufuzu michuano
ya Mataifa Afrika, sasa imetoa mpya nyingine.
Juzi kwenye mchezo wa Ngao ya
Jamii kati ya Yanga na Azam uliomalizika kwa Azam kuibuka na ushindi wa penalti
4-1, akaunti hiyo iliwekwa matokeo yaliyosemeka Azam imeshinda kwa penalti 4-2,
kitu ambacho si sahihi.
Championi ambalo lilikuwepo
uwanjani hapo, lilishuhudia dakika 90 zikimalizika kwa sare ya mabao 2-2 na
katika mikwaju ya penalti, Yanga ilipiga mitatu na kufunga moja huku Azam
ikipiga minne ambayo yote iliingia langoni.
Deogratius Munish ‘Dida’
ndiye aliyeifungia Yanga penalti hiyo, huku Hassan Kessy na Haruna Niyonzima
wakikosa na kwa upande wa Azam, John Bocco, Shomari Kapombe, Himid Mao na Kipre
Balou ndiyo waliofunga.
Hata hivyo, licha ya TFF
‘kuibeba’ Yanga kwa kuipa bao moja la bure la penalti, lakini haikusaidia
kuinyima Azam kutokuwa bingwa wa mchezo huo kwa mara yao ya kwanza baada ya
kushiriki mara tano mfululizo.
Post a Comment