KATIKA hali ya kushangaza mmiliki wa Klabu ya
African Lyon, Rahim Zamunda na Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba juzi
Jumamosi nusura warushiane makonde kufuatia matokeo ya timu zao ya sare ya bao
1-1 katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu
Bara uliopigwa usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar.
Mchezo huo ulionekana wazi kuwa mgumu kwa kocha
mpya wa Azam, Mhispania, Zeben Herenandez kutokana soka la hali ya juu
lililoonyeshwa na African Lyon iliyopanda daraja msimu huu ikiwa na kocha mpya
Bernardo Tevares.
Championi lilimshuhudia mmiliki huyo wa African
Lyon akianza kulalamika kufuatia kuongezwa kwa dakika sita za nyongeza katika
mchezo huo huku wakiongoza kwa bao 1-0 lililofungwa na Hood Mayanja kwa njia ya faulo, hali Iiliyozua
sintofahamu kwa upande wa timu hiyo kwani walidai kuonewa kutokana na
kuongezwa kwa dakika nyingi.
Hali
ilizidi kuwa mbaya kwa bosi huyo baada ya Azam kusawazisha bao lao kupitia
nahodha John Bocco wakati mshambuliaji wa African Lyon akiwa ameumia hali
iliyolazimu kwenda chini ya jukwaa kuu na kuanza kuwatuhumu viongozi wa Azam
wanabebwa, kitendo kilichomkera Kawemba ambaye alianza kumjibu kabla hajashuka
chini kabisa mpira ulipoisha kisha kuanza kujibizana kisharishari na kiongozi
huyo.
Ugomvi wa viongozi hao ulikuwa mkubwa
walipokutana katika eneo la kubadilishia nguo ‘dressing room’ za wachezaji
kutokana na kila mmoja kumtolea maneno ya kashfa mwenzake kabla ya polisi na
baadhi ya viongozi wengine kuingilia kati kuwatuliza kwa kuwaondoa kwenye eneo
hilo.
Hata hivyo, hakuna kiongozi ambaye alikuwa tayari
kuliongea hilo mara baada ya kuachanishwa.
Post a Comment