USIIONE Simba imekuwa tamu ukadhani benchi la ufundi
limeridhika! Katika kuhakikisha anatimiza ahadi yake ya kushinda kila mechi ya
Ligi Kuu Bara, kocha mkuu wa timu hiyo, Mcameroon, Joseph Omog, amekipangua
kikosi chake kidogo kwa kuwaingiza na kuwaondoa wachezaji watatu kwenye ‘First
Eleven’ yake.
Mabadiliko hayo ya kikosi chake yanatarajiwa kuonekana kwenye mechi ya
leo ya ligi kuu wakati timu hiyo itakapopambana na JKT Ruvu kwenye Uwanja wa
Uhuru jijini Dar es Salaam.
Wachezaji wanaotarajiwa kuingia kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo ni
Mganda, Juuko Murshid akipishwa na Novalty Lufunga huku Fredric Blagnon raia wa
Ivory Coast akimuondoa Ibrahim Ajib na Malika Ndeule akianza kuchukua nafasi ya
Hamad Juma aliyetereza chooni na kupasuka kichwani.
Katika mazoezi ya siku mbili waliyoyafanya Simba kwenye Uwanja wa Boko Beach
Veteran, Dar, Mcameroon huyo alionekana akipanga vikosi viwili huku kimoja
akionekana akikipa maelekezo na mbinu mbalimbali za ndani ya uwanja.
Kikosi hicho alichokuwa anakipa maelekezo kocha huyo ambacho huenda
kikaanza kwenye mechi ya leo dhidi ya JKT Ruvu kiliundwa na kipa, Vincent
Angban, Malika Ndeule, Mohammed Hussein Zimbwe, Juuko, Method Mwanjale, Jonas
Mkude, Jamal Mnyate, Mzamiru Yassin, Blagnon, Laudit Mavugo na Shiza Kichuya.
Wakati mazoezi hayo yanaendelea, washambuliaji Mavugo na Blagnon walionekana
wakicheza kwa kuelewana huku wakitengenezeana nafasi za kufunga mabao.
Katika mazoezi hayo, Blagnon alionekana kuwavutia mashabiki wa timu hiyo
waliofika kuangalia mazoezi baada ya bao lake safi la kichwa alilolifunga
akiunganisha krosi ya Kichuya.
Mara baada ya mazoezi hayo kumalizika, kocha huyo alizungumza na Championi Jumamosi na kusema: “Wala
usishangae kuona mchezaji aliyepo kwenye kikosi cha kwanza, kwenye mechi
inayofuata akaanzia benchi.
“Kikosi changu nitaendelea kukiimarisha kila kukicha na kikubwa ninataka
kuona kila mchezaji anaonyesha kiwango kizuri ndani ya uwanja pale anapopata
nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza.
“Kama mchezaji nikimpa nafasi ya kucheza na akashindwa kuitumia vema,
basi mechi ijayo usitarajie kumuona akicheza, nitampa nafasi mwingine na
kikubwa ninafurahia kuwa na kikosi kipana katika kikosi changu cha msimu huu,”
alisema Omog.
Post a Comment