YANGA leo
inaanza rasmi mikikimikiki ya Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kucheza na African
Lyon, ambapo tayari homa ya mpambano huo imepanda kwa watoto hao wa mjini,
wakiwahofia zaidi washambuliaji, Donald Ngoma na Amissi Tambwe.
Lyon ambayo
katika mchezo wa fungua dimba la michuano hiyo iliibana Azam FC kwa kulazimisha
sare ya bao 1-1 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, bado
inakumbuka uwezo wa Tambwe ambaye alimaliza msimu uliopita akiwa kinara wa
kupachika mabao na vile vile Ngoma ambaye ametokea kuwa straika hatari katika
kikosi cha Yanga.
Yanga
hawakuanza ligi mwishoni mwa wiki iliyopita kama timu nyingine kutokana na
kukabiliwa na michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na sasa wanarejea rasmi
wakianza na timu hiyo iliyorejea kucheza Ligi Kuu msimu huu baada ya kushuka
daraja 2012/13.
Uwezo wa
mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara unawafanya kuendelea kupewa
nafasi kubwa ya kutetea ubingwa wao sambamba na watani zao wa jadi Simba ambao
nao wameonekana kujipanga vizuri.
Licha ya
kwamba Kocha Mkuu wa African Lyon, Bernardo Tavares, kusema kuwa watafanya kila
liwezekanalo kuhakikisha wanawafunga Wanajangwani hao, bado wana hofu na uwezo
wa upachikaji mabao wa Ngoma na Tambwe ambao unatajwa kuwepo katika kambi ya
timu hiyo.
Kiwewe
wanachokipata African Lyon ni kutokana na uwezo waliouonyesha Ngoma na Tambwe
msimu uliopita ambapo Tambwe aliweza kuibuka mfungaji bora baada ya kupachika
mabao 21.
Yanga
watashuka dimbani wakiwa na hasira kubwa baada ya kushindwa kusonga mbele hatua
ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika na sasa
watataka kuona wanaanza vema michuano ya ligi.
Wanajangwani
hao wanajua kuwa wapinzani wao wa jadi Simba wamekalia usukani na sasa watataka
kufanya kila linalowezekana ili kuwashusha na kupunguza kelele za mashabiki wa
Wekundu hao wa Msimbazi.
Post a Comment