KOCHA wa Yanga Mholanzi, Hans van Pluijm, amesema moto walioanza nao katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu ni mkubwa lakini wachezaji wake wanatakiwa kuongeza kasi ili waweze kupata mabao mengi zaidi na ikiwezekana yafike 100.
Yanga ilianza vizuri msimu wa ligi Jumapili iliyopita kwa kuifunga African Lyon mabao 3-0, hali iliyomfurahisha Pluijm ambaye kwa sasa anatabasamu muda wote.
Kwa matokeo hayo, Yanga imekuwa miongoni mwa timu chache zilizocheza mechi zake za kwanza msimu huu bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa sawa na timu za Kagera Sugar, JKT Ruvu, Stand United na Mbeya City ingawa bado Wanajangwani hao wanatarajia kupata ushindi mwingine katika mechi zijazo.
Tayari Pluijm ametoa maagizo kwa nyota wake akiwataka kila mmoja kutafuta nafasi ya kufunga pindi anapopata upenyo bila kujali mchezaji anacheza katika nafasi gani.

Ametoa maagizo hayo huku akidai anataka kuvunja rekodi ya msimu uliopita ambapo walifanikiwa kufunga jumla ya mabao 70 na kuzipiku timu nyingine zote zilizoshiriki na hivyo kutwaa taji la ubingwa, huku ikiruhusu nyavu zake kuguswa mara 20 pekee.
Hata hivyo, Pluijm amesema pamoja na kutaka nyota wote wafunge lakini jukumu zito anawapa washambuliaji wake wanne ambao ni Amissi Tambwe, Donald Ngoma, Simon Msuva, Juma Mahadhi na Obrey Chirwa.
Wachezaji hao wamepewa majukumu hayo hivi karibuni baada ya kumweleza kocha huyo kuwa wapo tayari kubeba zigo hilo.
Akizungumza na DIMBA, mmoja wa nyota wapya aliyefunga bao la ‘rekodi’, Juma Mahadhi, alisema kuwa kocha amewapa jukumu hilo na anaamini watalimudu.
“Ametutaka sisi kuwa viongozi wa kuhakikisha tunafunga mabao 100 au zaidi kwenye ligi kuu msimu ujao.
“Amesema kama tukifunga idadi hiyo, basi tutakuwa na nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa huo mwishoni mwa msimu.

“Kutokana na hali hiyo kwa hesabu za haraka haraka, kila mmoja wetu anatakiwa afunge mabao 15, achana na yale yatakayofungwa na mabeki na viungo,” alisema.
Ujio wa Mahadhi pamoja na Chirwa endapo watatimiza majukumu yao ya kutikisa vyavu huenda ahadi hiyo ya Pluijm kuvuna mara mbili ya msimu uliopita ikatimia ambapo kihesabu ni sawa na jumla ya mabao 140.
Yanga ambayo inaendelea kujifua kwenye viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam, itashuka tena dimbani kucheza mchezo wao wa Ligi Kuu Agosti 7, mwaka huu dhidi ya Ndanda FC kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara, baada ya nyota wake kadhaa walioko kwenye timu za taifa za nchi zao kurejea kikosini.

Post a Comment

 
Top