SIMBA
wanatarajia kubisha hodi Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA), baada ya
Kamati ya Sheria, Hadhi ya Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),
kumuidhinisha beki wao wa zamani, Hassan Ramadhani ‘Kessy’ kuichezea Yanga
katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Uamuzi wa
Simba kwenda FIFA unatokana na malalamiko yao yaliyowasilishwa kwa kamati hiyo
dhidi ya Yanga kutupwa, huku Kessy akiidhinishwa Yanga.
Simba
waliwasilisha malalamiko kwa TFF wakidai Kessy kuwalipa Dola 60,000, sawa na Sh
milioni 126 kutokana na kuvunja mkataba uliokuwa umalizike Juni 15, mwaka huu.
Kiongozi wa
juu wa Simba, ambaye hakutaja jina lake liandikwe gazetini, alisema wanatarajia
kutinga FIFA, baada ya kutoridhika na uamuzi wa Kamati ya Sheria na Hadhi ya
Wachezaji TFF.
Kiongozi
huyo alisema kamati ya utendaji ya klabu hiyo ilitarajia kukutana jana jioni
kwa ajili ya kujadili pamoja na mambo mengine, uamuzi huo wa TFF kabla ya
kulipeleka FIFA.
Alisema
uamuzi wa kutafuta haki katika chombo kingine cha juu unatokana na malalamiko
yao mengi yanayowasilishwa TFF kupuuzwa.
Katika hatua
nyingine, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, alisema baada ya
kikao cha kamati ya utendaji jana, anatarajia kuzungumza na waandishi wa habari
kuhusu sakata la Kessy.
Kessy
alishindwa kuichezea Yanga kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, baada
ya Simba kuweka pingamizi kwa madai alikuwa hajamaliza mkataba.
Lakini
kamati ya Sheria, Hadhi na Wachezaji ya TFF, wiki iliyopita ilimuidhinisha
kuichezea Yanga, huku ikiwataka Simba kumalizana na Kessy.
Post a Comment