KAMA ulidhani Yanga watapoteana Ligi Kuu baada ya kupata
matokeo mabaya Kombe la Shirikisho Afrika, imekula kwako kwani Wanajangwani hao
wanapewa nafasi kubwa ya kutetea ubingwa wao.
Yanga wameyaaga mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika
baada ya kushika nafasi ya mwisho kwenye kundi lao na sasa wanarudi Ligi Kuu
wakiwa na hasira.
Kutokana na kucheza muda mrefu baadhi ya mashabiki na
wapinzani wa Yanga wanadhani kuwa wachezaji wa Yanga hawatakuwa kwenye ubora
wao, lakini wachambuzi wa soka wanasema kuwa hiyo imezidi kuwapa uzoefu.
Kocha na mchambuzi wa soka nchini, Kenny Mwaisabula ‘Mzazi’,
amesema kuwa uzoefu walioupata Yanga katika michuano ya kimataifa utawasaidia
sana kwenye ligi katika harakati za
kutetea taji lao msimu huu.
Mwaisabula alisema kuwa Yanga wamecheza mechi nyingi na
wamekaa pamoja kwa muda mrefu jambo ambalo litawafanya wawe kwenye ubora zaidi
wanaporejea kwenye Ligi Kuu kuliko watu wanaavyodhania.
“Ukiangalia timu zinazoshiriki kwenye ligi, nyingi
zimebadili kikosi, mabenchi ya ufundi hiyo itachukua muda kidogo kucheza kitimu
kwani hawajazoeana sana, tofauti na ilivyo kwa Yanga kwani hata wale wapya
waliowasajili hivi karibuni tayari wameshacheza mechi pamoja na hivyo kila
mmoja kumjua mwenzake,” alisema.
Kwa upande wa mchambuzi wa soka wa kituo cha Efm na gazeti
hili, Oscar Oscar, amesema kuwa Yanga wana nafasi kubwa ya kutetea taji lao
msimu huu licha ya kwamba kutakuwa na upinzani mkali kutoka kwa watani zao Simba
na pengine Azam.
“Kulingana na vikosi vilivyo msimu huu, Simba ndio wanaoweza
kuwasumbua kulingana na usajili wao lakini pia hivi sasa hawana tatizo la ukata
lililokuwa likiwatesa kwa muda mrefu hasa baada ya ujio wa mfanyabiashara,
Mohamed Dewji ‘Mo’ ambaye ameonyesha nia ya kuwekeza kwa Wekundu hao wa
Msimbazi.
“Mbali na hilo, Yanga wana nafasi ya kutetea taji lao kwani
kwa muda mrefu kikosi kipo pamoja na benchi la ufundi ni lile lile jambo ambalo
limewaepusha wachezaji kufanya mambo
ambayo yangeweza kuwafanya wasiwe kwenye ubora wao kama vile ulevi, kucheza
ndondo na kupata majeraha yasiokuwa na sababu za msingi,” alisema.
Alisema kuwepo kwao pamoja kunawafanya waendelee kuwa kwenye
ubora wao na kucheza soka la ushindani, lakini hilo litawezekana iwapo kocha
Hans van de Pluijm, atakuwa tayari kuwapumzisha wale wachezaji waliocheza mechi
nyingi na kuonekana kucheza na hivyo kutoa nafasi kwa waliokuwa nje kwa muda
mrefu.
“Iwapo kama Pluijm atakubali kuwapumzisha baadhi ya
wachezaji wanaoonekana kuchoka kutokana na kukosa muda wa kupumzika na
kuwatumia wengine, ataweza kuwa na kikosi cha ushindani lakini akiendelea na
yale maamuzi yake ya kuwang’ang’ania wale wale basi tusitegemee ushindani
mkubwa kutoka Yanga kwani wachezaji hivi sasa ni wazi wamechoka na wanahitaji
muda wa kupumzika, ingawa Yanga wana kikosi kipana zaidi na kilichojaa
wachezaji mahiri,” alisema.
Aidha, kocha Fred Minziro, alisema wanatagemea Yanga itakuwa
imepata uzoefu kutokana na kuwa mashindano waliyoshiriki ni makubwa kuliko Ligi
Kuu Tanzania Bara.
Alisema Yanga wataingia kwenye ligi wakiwa na nguvu mpya
hasa ukizingatia wametoka kupambana na timu ngumu ukilinganisha na zile
zinazoshiriki ligi.
“Kwa maoni yangu watakuja wakiwa vizuri zaidi lakini
ushindani utakuwepo licha ya uzoefu walioupata, uchovu utawaathiri kwa sababu
wamecheza kwa muda mrefu bila kupumzika na wakirudi wanaingia moja kwa moja
kwenye ligi,” alisema Minziro.
Kwa upande wake kocha wa timu ya Taifa, Charles Mkwasa,
alisema Yanga licha ya kutolewa katika hatua hiyo wamejifunza vitu vingi
vitakavyowasaidia kwenye mechi za Ligi Kuu.
Alisema mashindano waliyoshiriki yamekuwa katika ushindani na timu kubwa hivyo
wataingia kwenye ligi wakiwa wanajiamini zaidi.
Hata hivyo, Mkwasa alisema Yanga itakutana na
changamoto za upinzani kutoka kwenye
timu watakazokutana nazo katika ligi ambapo kila mmoja atataka kuonyesha uwezo
wake.
“Yanga watakutana na vikwazo vya wapinzani ambao watakuwa
wanacheza kwa kujituma zaidi kupata
matokeo mazuri na kutaka kama kuwatoa
Yanga nishai ili kudhihirisha ubora wao, kwamba nao wanaweza kukabiliana hata kama hawajashiriki michuano mikubwa,”
alisema Mkwasa.
ChanZO: Bingwa
Post a Comment