WAKATI Kocha wa Yanga, Hans van
Der Pluijm akiendelea kuumiza kichwa juu ya kutibu tatizo la upigaji penalti
ndani ya kikosi chake, tayari mpinzani wake, Kocha wa Simba, Joseph Omog amedai
kuwa ameshapata dawa hiyo na hana wasiwasi.
Yanga imekuwa na tatizo hilo kwa
muda mrefu sasa kiasi cha kukosa nafasi nyingi ikiwemo hivi karibuni ambapo
Azam FC ilitwaa ubingwa wa Ngao ya Jamii kwa kuifunga Yanga kwa penalti 4-1.
Omog ameliambia Championi
Ijumaa kuwa, katika kikosi chake, hana wasiwasi kabisa endapo watapata penalti
kwenye mechi zao kwani anao wapigaji wanne wenye uwezo wa hali ya juu kufunga
kiufundi.
“Nina wachezaji wanne wenye
uwezo mkubwa wa kupiga penalti na hao ninawaamini hawawezi kuniangusha endapo
itatokea tumepata penalti kwenye mechi zetu, siwezi kuyaweka wazi majina yao
kwa sasa, lakini siku ukiona tumepata penalti, basi atakayepiga ndiye mmojawao,”
alisema Omog.
Ikumbukwe kuwa, msimu
uliopita, Simba ilikuwa ikiwategemea Ibrahim Ajib na Hamisi Kiiza kwenye
upigaji penalti, huku jukumu la upigaji faulo na kona likiwa chini ya Mohammed
Hussein ‘Zimbwe Jr’ ambapo pia msimu huu anaendelea na jukumu lake hilo.
Katika mchezo uliopita dhidi
ya Azam FC, wachezaji wa Yanga waliokosa penalti ni Hassan Kessy na Haruna
Niyonzima.
Post a Comment