BEKI wa Yanga SC, Hassan Kessy aliyekosa
penalti na kushuhudia Yanga ikifungwa kwa penalti 4-1 dhidi ya Azam katika
mechi ya Ngao ya Jamii, juzi alijikuta akibaki na mshangao kwa kile alichofanyiwa
na Wanayanga mara baada ya mchezo huo.
Kessy ambaye alijua anaweza kupata lawama nyingi kwa kukosa penalti katika
mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, anasema kuwa alipigiwa simu
nyingi na mashabiki wa Yanga waliokuwa wakimfariji.
"Naomba niwaombe radhi Yanga kwa kukosa penalti, ukweli ni kuwa ile
mechi tulitakiwa kuimaliza mapema kwa kuwa tulitawala mchezo huo lakini ndiyo
hivyo.
“Nashukuru mashabiki wa Yanga kwa kunipigia simu kujifariji na kunitia moyo
baada ya kukosa penalti, niwaambie kuwa tupo pamoja," alisema Kessy na
kuongeza:
“Siwezi kuzungumzia sana namna nilivyokosa
lakini najisikia vibaya kwa kweli, inaniuma sana.”
Aidha, akizungumzia kuhusu kumwaga machozi
mara kadhaa katika mchezo huo, Kessy alisema: “Nalia kwa sababu ya furaha kwani
sikuamini kabisa kama ningeitumikia Yanga kwa sababu kila mtu anajua nini
kinachoendelea dhidi yangu.
“Tangu nimetua Yanga nimekumbana na vizingiti
vingi sana ambavyo vimenifanya nishindwe hata kucheza mechi za kimataifa ila
naamini Mungu yupo na kila kitu kitakaa sawa,” alisema.
Post a Comment