MSHAMBULIAJI wa Yanga, Mrundi, Amissi Tambwe,
ameamua kuweka wazi sababu za kukabiliwa na ukame wa mabao hasa katika michuano
ya kimataifa kuwa kikubwa ni kubadilishiwa majukumu uwanjani.
Tambwe, mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu
uliopita, amesema kuwa zamani alikuwa akichezeshwa kama mshambuliaji wa kati
namba tisa lakini kwa siku za hivi karibuni amekuwa akipangwa kucheza namba 10
akiwa nyuma ya straika, hali inayomfanya kuwa mbali na lango.
“Ni kweli mimi mwenyewe najiona nimepunguza
kasi ya kufunga, nafikiri sababu kubwa ni mabadiliko hayo ya nafasi uwanjani,
namba kumi inaniweka mbali na lango, hiyo inatokana na mfumo wa kocha
tunaotumia kwa sasa.
“Kwa nafasi hiyo siwezi kufunga sana, japokuwa
nitajitahidi kufanya hivyo lakini haitakuwa kama awali, ndiyo maana hata sasa
hivi sionekani sana kwenye boksi la timu pinzani, kwa hiyo hata msimu ujao
itategemea na kocha atakavyonitumia.
“Siwezi kupinga chochote kulingana na maagizo
hayo ya kocha kwa kuwa yeye ndiye anayetambua umuhimu wangu na anaendelea
kunipanga anapoona ni sahihi, mimi nitaendelea kutekeleza majukumu ninayopewa
kama kawaida,” alisema Tambwe.
Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm, amekuwa
akimkabidhi majukumu ya namba tisa, Mzimbabwe, Donald Ngoma au Obrey Chirwa
tofauti na awali ambapo hao walikuwa wakicheza nyuma ya Tambwe au pembeni.
Post a Comment