YANGA
ikiwa inatafuta ushindi kwa udi na uvumba katika mechi yake inayokuja dhidi ya
Waarabu wa Algeria, MO Bejaia, imejikuta ikimpoteza na kushindwa kumtumia
straika wake hatari, Mzimbabwe, Donald Ngoma.
Yanga
itashindwa kumtumia mshambuliaji wake huyo aliyefunga mabao manne mpaka sasa
katika michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho Afrika kutokana na adhabu ya kadi
mbili za njano ambayo kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Afrika (Caf), mchezaji
anapaswa kukosa mchezo unaofuata.
Ngoma
alipata kadi ya pili katika mchezo wao dhidi ya Medeama uliopigwa nchini Ghana
na kufungwa kwa mabao 3-1. Mwingine aliyepata kadi katika mchezo huo ni Nadir
Haroub ‘Cannavaro’, yeye atacheza dhidi ya Bejaia lakini anapaswa kujichunga
asipate nyingine ya pili.
Kutokana
na hilo, Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm, amesema Ngoma ni mchezaji muhimu
lakini kwa kuwa ana kikosi kipana hakuna tatizo katika hilo, ataiziba nafasi
hiyo siku hiyo na kila kitu kitakwenda sawa.
Yanga
inatarajia kuvaana na Bejaia Agosti 13, mwaka huu, katika Uwanja wa Taifa, siku
ambayo pia Mwanamuziki wa Tanzania, Fareed Kubanda ‘Fid Q’ atakuwa
anasherehekea siku yake ya kuzaliwa.
“Katika
mechi ya Bejaia nitamkosa Ngoma tu kutokana na kadi mbili za njano alizonazo,
kweli ni mchezaji mzuri lakini kwa kuwa nina kikosi kipana hapa, hakuna
kitakachoharibika, tutawatumia waliopo kwa ajili ya kuipigania timu,” alisema
Pluijm, raia wa Uholanzi.
Katika
michuano hiyo, hii ni mara ya pili, Ngoma anakaa nje kutokana na adhabu ya kadi
mbili za njano, awali alikosekana katika mechi iliyopigwa Uwanja wa Taifa, Dar
dhidi ya Cercle de Joachim ya Mauritius.
Beki
Vicent Bossou naye alipata kadi kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Medeama na ule
wa pili uliopigwa Ghana hakucheza kwa kuwa alikuwa akitumikia adhabu hiyo.
Post a Comment