WAKATI timu nyingine zikiendelea kujiimarisha kwa kufanya usajili, Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger, amewashangaza watu baada ya kudai kuwa haoni wachezaji wanaofaa kuwasajili katika soko la sasa.

Arsenal imefanikiwa kufanya usajili wa mchezaji mmoja tu msimu huu, Granit Xhaka na kocha huyo amesema sasa haoni mwingine wa kumsajili.

Kocha huyo raia wa Ufaransa amesema atamsajili mchezaji ambaye anaweza kukisaidia kikosi chake tu na siyo vinginevyo.

Arsenal inatakiwa kumsajili beki wa kuziba pengo la Per Mertesacker ambaye ana majeraha yatakayomweka nje ya uwanja hadi mwakani lakini inahitaji pia mshambuliaji mmoja.

"Nitasajili mchezaji ambaye naamini anaweza kukisaidia kikosi changu. Siku hizi unatakiwa kuwa mtu makini sana kama unataka kufanya usajili kwenye klabu siyo suala la kununua tu.

"Kuna mawazo mengi sana kuhusu wachezaji siku hizi, naweza kusema kuwa sasa watu wanamfahamu kila mchezaji mzuri.

"Wanakaa wanasema kuwa kocha unatakiwa kununua, lakini ukiwauliza umnunue nani wanakuwa tena wapole hawana wa kukuambia umnunue.

"Ukitazama Ulaya kwa sasa utawaona wachezaji wengi waliosajiliwa hawawezi kuzibeba klabu zao. Ukiangalia timu ambazo zinatoa pesa nyingi mno kwenye usajili, siyo zile ambazo ni lazima zitwae ubingwa.

“Uwekezaji wa klabu kwa kusajili kwa pesa nyingi, haukuweza kuizuia Leicester kutwaa ubingwa. Mimi nitasajili mchezaji anayeweza kuisaidia timu hii tu,” alisema Wenger.

Hata hivyo, kocha huyo amesema kuwa bado timu yake ipo kwenye usajili na akipata mchezaji mzuri atamsajili.


Post a Comment

 
Top