OFISA Habari wa Simba, Haji
Manara, hivi karibuni alipata matatizo ya macho baada ya jicho lake moja
kupoteza uwezo wa kuona, wakati akiendelea na matibabu, wanachama wa Yanga
wameamua kumchangia fedha za matibabu katika kile walichodai kuonyesha michezo
siyo uadui.
Wanachama hao wameongozwa na Mkuu
wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro ambaye alithibitisha
juu ya mchango huo kwa kusema kuwa wamefikia uamuzi huo kutokana na kuguswa
zaidi na tatizo hilo ambalo limempata Manara kama ndugu na mdau mkubwa katika
soka nchini.
“Soka siyo uadui bali ni mchezo
unaotuweka pamoja, pia upinzani wa Simba na Yanga upo uwanjani ila nje ya
uwanja sisi sote ni ndugu, tatizo alilopata Manara ni kubwa.
“Kutokana na hali hiyo tukiwa
kama wanafamilia wenzake na ndugu zake imetubidi tuchangishane ili kuhakikisha
tunapata kiasi fulani cha fedha kitakachomsaidia katika matibabu yake.
“Tumepanga kuwa kama ataenda nje
ya nchi basi gharama zote za nauli ya kwenda na kurudi ziwe kutoka kwa
wanachama na mashabiki wa Yanga, hata hivyo mpaka sasa tumeshachangishana zaidi
ya shilingi milioni moja na bado tunaendelea,” alisema Muro na kuongeza:
“Fedha hizo tutamkabidhi siku
yoyote ile kuanzia leo mara tu tutakapokutana kwa pamoja na waratibu wa zoezi
hili.”
Alipotafutwa Manara ili aweze
kuzungumzia suala hilo hakuweza kupatikana kufuatia simu yake ya mkononi kuita
tu bila ya kupokelewa.
Post a Comment