BENCHI jipya la ufundi la Azam FC linaloongozwa na Wahispania watano na Mbongo, Denis Kitambi, limekuja na falsafa ya kipekee kikosini hapo, baada ya kutangaza kufuta usajili wa kikosi kizima na kuanza moja kabisa kusaka wachezaji wengine.

Benchi hilo lililo chini ya Kocha Mkuu Zeben Hernandez akisaidiana na Wahispania wenzake wanne wote kutoka Tenerife ya nchini kwao, limetoa msimamo huo ikiwa na maana hata wachezaji mastaa wa kikosi hicho, John Bocco na Kipre Tchetche nao wanalazimika kuonyesha uwezo ili wapate namba.

Makocha wengine ni kocha msaidizi Yeray Romero, Pablo Borges (kocha wa makipa) na kocha wa viungo, Jonas Garcia.

Azam ilianza rasmi mazoezi jana Alhamisi katika uwanja wao wa Chamazi Complex ambapo pia wale waliokuwa kwa mkopo msimu uliopita kama Kelvin Friday (kutoka Mtibwa), Omar Wayne (Coastal Union) na Joseph Kimwaga (Simba) nao wakiwa mazoezini.

Msemaji wa kikosi hicho, Jaffar Idd Maganga ameliambia Championi Ijumaa kuwa, kocha alitoa pendekezo ya kuanza na moja kwani benchi zima haliwajui wachezaji wao, hivyo kutoa nafasi ya kukiangalia upya kikosi kwa muda wa siku 15 kabla ya kutangaza akina nani watasalia kikosini.

“Kwa sasa kila mmoja ana nafasi ndani ya Azam na baada ya muda mwalimu alioomba (siku 15) ndipo tutajua Azam ya msimu ujao itakuwa na wachezaji aina gani,” alisema Idd.

Kipre matatani Azam
Idd aliongeza kuwa wanafanya kila njia kupata sababu za mshambuliaji wao, Muivory Coast, Kipre Tchetche kutorejea kikosini mpaka jana kinyume na taratibu ambapo alitakiwa kuwa kikosini.

“Kipre bado ni mchezaji wetu, ana mkataba wa mwaka mmoja hivyo hawezi kwenda popote na bahati nzuri hata ITC yake tunayo sisi, kwa hiyo tunajaribu kufanya mawasiliano kujua sababu ya kuchelewa kambini na kinyume cha hapo atachukuliwa hatua,” alisema Idd.

Naye pacha wa nyota wa Kipre, Michael Bolou alipoulizwa na gazeti hili kuhusu alikomuacha mwenzake alijibu kwa kifupi: “Mimi nilimuacha nyumbani, mengine sifahamu lolote.”

Post a Comment

 
Top