Miniger

MJIPANGE siyo siri kwani straika Ibrahima Fofana wa Ivory Coast ameanza vizuri majaribio yake katika kikosi cha Azam FC na jana klabu hiyo imemleta mshambuliaji mwingine Mossi Moussa Issa kutoka Niger kwa kujaribiwa.
Fofana katika mazoezi ya Azam jana asubuhi kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar, alionyesha uwezo mkubwa kucheza zaidi ya nafasi tatu uwanjani.
Kocha wa Azam, Zeben Hernandez, ameonyesha kuridhishwa na uwezo wa Fofana katika kutoa pasi na kushambulia kwa nguvu.
Fofana ana umri wa miaka 26 na ametokea katika Klabu ya Union Sportive de Ben Guerdane ya Tunisia aliyokuwa akiichezea msimu uliopita, kabla ya kujiunga na timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Tunisia (Ligue 1).
Straika huyo alikuwa mwiba mara baada ya kocha kuwagawa wachezaji katika vikosi viwili ambapo muda mwingi alicheza winga ya kushoto na alikuwa akimsumbua beki Erasto Nyoni kutokana na kasi yake.
Kuhusu Fofana, Kocha Zeben alisema: “Nimemuona anaendelea vizuri lakini nitazidi kumtazama ili kujiridhisha na uwezo wake, maana ndiyo namuona kwa mara ya kwanza.”
Wakati huohuo, Azam imemleta straika mwingine Mossi Moussa Issa mwenye miaka 22 kutoka Niger kwa ajili ya majaribio. Issa anatokea Sahel Sporting Club inayashiriki Ligi Kuu ya Tunisia. Huyu anaanza kujaribiwa leo Jumamosi.
Mbali na wachezaji hao, jana mchana Azam ilimshusha daktari Mhispania, Sergio Soto Perez anayekuwa mkuu wa kitengo.

Post a Comment

 
Top