![]() |
MATOLA |
SIKU
chache tangu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilipotangaza majina ya
wanaowania tuzo mbalimbali za Ligi Kuu Bara 2015/16, baadhi ya makocha wazoefu
wamekosoa na wengine kusifia kwa wanaowania tuzo hizo zitakazotolewa Julai 17,
mwaka huu.
Kocha
wa zamani wa Simba, Selemani Matola amepongeza uteuzi wa wanaowania tuzo ya
kocha bora kuwa walistahili lakini akakosoa uteuzi wa wanaowania mchezaji bora
wa kigeni ambao ni Wazimbabwe, Thabani Kamusoko na Donald Ngoma wote Yanga na
Muivorycoast, Vincent Angban wa Simba.
Wanaopigania
tuzo ya kocha bora ni Mholanzi, Hans van Der Pluijm wa Yanga, Mecky Maxime
(Mtibwa Sugar) na Salum Mayanga wa Prisons.
![]() |
JULIO |
“Kwa
makocha naona sawa ila tu wasifanye makosa kama yaliyopita, kama anastahili
mgeni wampe mgeni na kama anafaa mzawa basi wampe kwa vigezo kweli,
wasipendelee,” alisema Matola na kuongeza:
“Kwa
wachezaji wa kigeni naona siyo sawa kuwepo Angban, kuna watu walipaswa kuwepo
kama Kipre Tchetche (Azam) au Tambwe (Amissi, Yanga).
“Sijajua
wametumia vigezo gani lakini Angban amekuja katikati ya msimu, Tchetche au
Tambwe kila mmoja ameona shughuli yake, walifaa kuwepo sijui kwa nini hawapo.”
Kocha
wa zamani wa Yanga, Fred Minziro alisema: “Kwa kocha naona Mzungu (Pluijm)
anastahili, timu yake ipo kwenye kiwango kikubwa, imetwaa ubingwa wa ligi, Kombe
la FA na bado anaiwakilisha nchi kimataifa.
“Hawa
wa kigeni anastahili kupewa Ngoma. Tambwe hayupo lakini naona ni sawa kwa kuwa
unaweza kuwa mfungaji bora lakini usiwe kwenye kiwango cha juu, kuna kipindi
alipotea kidogo hapa katikati kabla ya kurejea mwishoni mwa ligi.”
Jamhuri
Kihwelo ‘Julio’, kocha wa Mwadui FC naye alisema: “Vyovyote naona sawa maana
hizi tuzo huwa wanapanga kwa hisia na si vigezo, mwaka jana walikosea wakampa
Makata (Mbwana) na mwaka huu naona vilevile tu.
“Sijisifii
lakini kocha bora nastahili mimi, ukiangalia nimeingia ligi kuu kwa mara ya
kwanza, nimemaliza nafasi ya sita, nimekwenda mpaka nusu fainali ya Kombe la FA
na yote hayo nimeyafanya bila ya mchezaji wa kigeni hata mmoja, lakini bado tu
haitoshi.”
Mbali
na tuzo hizo, nyingine 11 zitatolewa siku hiyo ni ya ubingwa wa ligi, makamu
bingwa, mshindi wa tatu, mshindi wa nne, timu yenye nidhamu, mfungaji bora,
mchezaji bora wa ligi, kipa bora, mchezaji bora chipukizi, bao bora la msimu na
mwamuzi bora.
Post a Comment