WAKATI uongozi wa Simba ukitarajiwa kutangaza kikosi chake leo Jumatatu kwa ajili ya msimu ujao wa 2015/16, mchakato huo umepigwa ‘stop’ kwa muda kutokana na mapendekezo ya kocha wao mpya, Joseph Omog raia wa Cameroon.
Omog ametoa angalizo hilo kwa kile kilichoelezwa kuwa anahitaji kuwaona wachezaji wakicheza kisha ndiyo atajua wale wanaoweza kubaki kikosini na wale ambao anaweza kuwatema.
Agizo hilo linamaana kuwa hata mchezaji wao mpya raia wa Ivory Coast, Blagnon Goue Fredric, ambaye ameshatua nchini kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya usajili naye atalazimika kutopewa mkataba kwa kuwa Omog anahitaji kuona uwezo wake uwanjani pamoja na Mcongo, Janvier Besala Bokungu naye atatakiwa kuonana kwanza na kocha huyo.
Bosi mmoja wa juu wa Simba ameliambia Championi Jumatatu kuwa angalizo hilo limeendana na ombi lake la kutotaka kuwa na mazoezi ya gym kwa sasa kama ambavyo imekuwa kawaida ya timu hiyo kufanya mwanzoni mwa msimu kabla ya mazoezi ya uwanjani.
“Huyu Mcongo hataweza kusaini mkataba na kiongozi yeyote hadi pale kocha atakapojiridhisha kuwa ana ubora wa kutosha.
“Lazima aingie mazoezini kocha aone uwezo wake ingawa viongozi wanaamini kuwa ni mchezaji mahiri lakini kocha ndiye mtu wa mwisho kwa sasa, sawa na kwanza Muivory Coast aliyetua jana (juzi).
“Kutokana na hali hiyo ndiyo maana imebidi tuanze mazoezi mapema ili aweze kuwaona wachezaji tuliowasajili kama wana sifa kweli za kuitumikia Simba.
“Tunatarajia kuanza mazoezi Jumatatu (leo), kocha ametuambia kuwa katika kutambua mchezaji gani ni mzuri na yupi hafai hilo halihitaji mtu kuwa fiti hata kama hana mazoezi yeye atajua na baada ya hapo ndipo atakapoanza kumjenga ili aweze kuwa sawa.
“Kutokana na hali hiyo tumekubalia kwa pamoja hivyo kikosi chetu tutakitangaza baadaye baada ya kocha kumaliza kazi yake hiyo,” alisema bosi huyo.
Uamuzi wa kuzuia mazoezi ya gym umeonekana mpya klabuni hapo kwa kuwa imekuwa ni kawaida kufanya hivyo bila kujali wanaye kocha mkuu au hawana, pia kitendo cha kuzuia usajili kinaonyesha jinsi ambavyo Mcameroon huyo hataki utani na yupo ‘serious’ na kazi yake.
Aidha katika mazoezi hayo ambayo hata hivyo Championi Jumatatu ilielezwa yanatarajiwa kuanza baada ya sikukuu na siyo leo, Omog anataka kusiwe na mashabiki labda waandishi kwa kuwa hataki kuwapotezea wachezaji umakini.
“Alituambia kuwa kama mazoezi hayo yatafanyika kwenye uwanja wenye mashabiki wengi atashindwa kuifanya kazi yake kwa ustadi mkubwa.
“Kutokana na hali hiyo ndiyo maana mpaka sasa bado sijajua mazoezi hayo tutayafanyika katika uwanja gani,” alisema mtoa taarifa huyo.

Post a Comment

 
Top