KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, Makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu' juzi alivamia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo vya Uwanja wa Taifa na kwenda kumpongeza kipa wa Medeama ya Ghana, Daniel Agyei.
Tukio hilo la aina yake lilitokea mara baada ya kumalizika kwa mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika wakati Yanga ilipowakaribisha Medeama na kubanwa kwa sare ya bao 1-1.
Katika mechi hiyo, kipa wa Medeama ndiye alikuwa kikwazo kwa Yanga kupata ushindi baada ya kuokoa mabao manne ya wazi akiwa yeye na Obrey Chirwa, Amissi Tambwe na Donald Ngoma aliyekosa mawili.
Kaburu baada ya kipyenga kupulizwa, akiwa amekaa jukwaa kuu la uwanja huo, haraka alishuka chini na kwenda kuingia kwenye vyumba vya Medeama na kumpongeza.
Hiyo haikutosha, Kaburu alimtoa nje ya vyumba hivyo na kumpa mkono wa kumpongeza huku akisikika akisema:
"Katika mechi ya leo wewe ndiye mchezaji bora, kiukweli unahitaji pongezi kubwa kutokana na kiwango kikubwa ulichokionyesha.
"Uliokoa hatari nyingi golini kwako ambazo kama siyo jitihada zako, basi mngefungwa, nakupongeza sana kwa kweli,” alisikika Kaburu akisema hayo.
Kaburu hakuishia hapo, alionekana muda mwingi mlangoni mwa vyumba vya Medeama huku akionyesha tabasamu zito la furaha baada ya Yanga kutoa sare hiyo.

Post a Comment

 
Top