BEKI wa kati wa Yanga, Mtogo, Vincent Bossou, amenasa kwenye mtego wa kufungiwa kucheza mechi moja na Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kutokana na kuwa na kadi mbili za njano.
Bossou ambaye kwa siku za hivi karibuni amekuwa tegemeo kubwa kwenye safu ya ulinzi ya Yanga, juzi Jumamosi kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Medeama uliopigwa katika Uwanja wa Taifa, Dar, alionyeshwa kadi ya njano, hivyo ataukosa mchezo wa marudiano unaotarajiwa kupigwa Julai 26, mwaka huu nchini Ghana.
Bossou alipewa kadi ya kwanza kwenye mchezo dhidi ya MO Bejaia uliopigwa Juni 19, mwaka huu nchini Algeria, ambapo Yanga ilikubali kichapo cha bao 1-0.
Awali, Yanga ilikuwa na wachezaji saba wenye kadi za njano ambao kama wangepewa tena kwenye mchezo huo wa juzi Jumamosi, basi ni lazima wangeukosa mchezo ujao wa marudiano na timu hiyo.
Wachezaji hao ni Deogratius Munish ‘Dida’, Kelvin Yondani, Mbuyu Twite, Haruna Niyonzima, Donald Ngoma, Thabani Kamusoko na Bossou.
Kutokana na kukosekana kwa Bossou, nahodha wa kikosi hicho, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ anaweza kurudi uwanjani kuchukua nafasi hiyo baada ya mara ya mwisho kuonekana kwenye mchezo dhidi ya Esperanca Sagrada ya Angola ambapo alionyeshwa kadi nyekundu.

Post a Comment

 
Top