MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Ivory Coast, Kipre Tchetche
huenda akaichezea klabu ya Simba msimu ujao baada ya uongozi wa timu hiyo kuwa
na mazungumzo ya chini kwa chini na mchezaji huyo aliyefanya vizuri katika
msimu minne aliyocheza Ligi ya Tanzania Bara.
Tchetche hajawasili kambini kujiunga na timu yake kwenye
maandalizi ya msimu ujao huku uongozi wake ukiwa hauna taarifa zinazomfanya
mchezaji huyo kushindwa kujiunga na wenzake kwenye maandalizi hayo.
Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Simba Geofrey Nyange ‘Kaburu’
alisema Tchetche ni mchezaji mzuri na wangependa kuwa naye, lakini hawezi
kulizungumzia hilo kwa sababu wapo watu wanaohusika na zoezi la usajili.
“Timu kubwa kama Simba siku zote inahitaji wachezaji wenye
kiwango na ubora wa juu kama Tchetche, ukizingatia hiki ni kipindi cha usajili
na tupo kwenye mazungumzo na idadi kubwa ya wachezaji ingawa hilo siwezi
kulisemea kwa sababu ipo kamati yetu ya usajili inahusika na hilo na
itatufahamisha baada ya kukamilisha kazi yake,”alisema Kaburu.
Kiongozi huyo alisema mipango yao kama uongozi ni kuijenga
upya timu hiyo kupitia kipindi hiki cha usajili ili kuweza kurudi kwenye
ushindani wa mbio za ubingwa kama ilivyokuwa siku za nyuma.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Azam FC, Nassor Idrissa,
alisema wanachojua mchezaji huyo bado ni mali yao kwa sababu bado ana mkataba
wa mwaka mmoja kuichezea timu yao, hivyo amezionya timu zinazomhitaji kufuata
taratibu na kanuni zinazotakiwa.
“Mimi ningezitaarifu klabu zinazomhitaji Tchetche, ikiwemo
Simba ambayo wanatajwa kuja mezani tuweze kujadili na kukubaliana ili tuweze
kuwaachia kwa sababu Simba ni watu wetu wa karibu na tumeshafanya nao biashara
ya kupeana wachezaji mara kadhaa sijaona kikwazo kinachowafanya washindwe kuja
mezani,”alisema Idrissa.
Post a Comment