MECHI ya Kundi A
Kombe la Shirikisho Afrika kati ya wenyeji, Yanga SC na Medeama ya Ghana
itachezwa Jumamosi ya Julai 16, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa na Mkuu
wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga, Jerry Muro leo.
Muro amesema tayari
wamekwishatuma taarifa za muda na siku ya kuchezwa mechi hiyo Shirikisho la
Soka Afrika (CAF) na hawana shaka mambo yatakuwa kama yalivyopangwa.
Yanga imejitahidi
safari hii kuitaarifu mapema CAF juu ya siku na muda wanaotaka kucheza mechi
yao, baada ya kujikuta wakicheza mechi iliyopita dhidi ya TP Mazembe kinyume na
matakwa yao.
Yanga ilifungwa 1-0
na Mazembe ya DRC Jumanne ya Juni 28, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
katika mchezo waliotaka wacheze Jumatano usiku.
Hata hivyo, CAF
iliwakatalia Yanga kuupeleka mbele mchezo huo kwa kuwa walichelewa kutuma
taarifa za mabadiliko – na mechi dhidi ya Mazembe kama wasingetoa taarifa
mapema ingechezwa Jumapili ya Julai 17.
Yanga itakuwa inasaka
ushindi wa kwanza katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Julai 16,
baada ya kupoteza mechi zote mbili za kwanza, mbali na Mazembe, pia walifungwa
1-0 na MO Bejaia nchini Algeria Juni 19, mwaka huu.
Post a Comment