UONGOZI
wa Simba umethibitisha kupokea barua kutoka Yanga ya kuomba barua ya
kumuidhinisha beki wao wa pembeni, Hassan Kessy kuichezea timu hiyo kwenye
msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho Afrika.
Beki huyo, hivi karibuni alizua mijadala
kwenye timu hizo kongwe wakati moja ikisema imepeleka barua ya kuomba
kuidhinishwa huku nyingine ya Simba ikikana kupokea barua hiyo.
Kessy hadi hivi sasa hivi amekosa michezo
miwili ya Kombe la Shirikisho Afrika ambayo ni dhidi ya MO Bejaia na TP Mazembe
kutokana na kutopata barua ya kuidhinishwa kutoka Simba.
Kanuni za Shirikisho la Soka Afrika (Caf)
zinaitaka Simba kutoa barua hiyo ndipo Yanga imtumie Kessy.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Rais
wa Simba, Evans Aveva, Jumatano wiki hii walipokea barua kutoka Yanga wakiomba
barua ya kumuidhinisha beki huyo ili wamtumie kwenye michuano ya kimataifa.
Aveva alisema, suala hilo limefikia kwenye
hatua nzuri za kumuidhinisha Kessy ili aichezee Yanga katika Kombe la
Shirikisho la Afrika.
Aliongeza kuwa, uamuzi wa kumuachia beki huyo,
utaenda sambamba na kikao cha Kamati ya Utendaji ya Simba itakapokutana na
kulijadili suala hilo kabla ya kuipatia Yanga barua ya kumuidhinisha.
“Nikuhakikishie tu, suala la Kessy limefikia
pazuri kwa maana ya kumruhusu kuichezea Yanga kwa kumpatia barua ya
kumuidhinisha kuichezea Yanga kwenye michuano ya kimataifa.
“Sidhani kama ni vizuri kumzuia Kessy, kikubwa
tulipokea barua kutoka Yanga ikiomba tuwapatie barua ya kumuidhinisha Kessy
aichezee timu yake hiyo mpya.
“Hivyo suala hilo siyo la kwangu pekee
linahusisha kamati nzima ya utendaji, kamati imepanga kukutana hivi karibuni
kwa ajili ya kujadiliana suala hilo na kufikia muafaka mzuri,’ alisema Aveva.
Aidha, alipotafutwa Katibu Msaidizi wa Chama
cha Wachezaji wa Soka Tanzania (Sputanza), Abeid Kasabalala kuzungumzia suala
hilo, alisema: “Tumewasilisha barua TFF ya kuomba kutoa kibali cha kumruhusu
Kessy kuanza kucheza, pia Simba na Yanga kukaa pamoja kulimaliza tatizo hilo na
siyo kutunishiana misuli.”
Post a Comment