YANGA jeuri sana kwani matajiri wa timu hiyo wamewapa wachezaji wa kikosi hicho Sh milioni 10 wagawane kwa ajili ya kununua vocha za simu na matumizi mengine madogomadogo.
Lengo la matajiri hao ambao ni wanachama wa Yanga ni kuwaweka sawa wachezaji ili washinde mechi ya leo ya Kundi A ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Medeama SC ya Ghana.
Matajiri hao wakiongozana na Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Isaac Chanji, Abdallah Bin Kleb, Husseni Nyika, Ahmed ‘Ndama’ na Mustapha Ulongo (aliyemsainisha Obrey Chirwa) walivamia kwenye mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika juzi jioni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kutoa kiasi hicho cha fedha.
Matajiri hao walifika uwanjani hapo dakika chache kabla ya Yanga kuanza mazoezi na baadaye walifanya kikao cha muda mfupi wao wenyewe na kupanga mipango ya kushinda mechi ya leo dhidi ya Medeama.
Wakiwa uwanjani hapo, mabosi hao walionekana wakifuatilia mazoezi hayo kwa makini na baadaye mara baada ya mazoezi kumalizika, walifanya kikao na benchi la ufundi la timu hiyo na wachezaji.
Championi Jumamosi, lilishuhudia nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ akikabidhiwa bahasha yenye rangi ya kaki ambayo baadaye ilielezwa kuwa ilikuwa na Sh milioni 10 ndani yake.
“Tumekuja mazoezi ghafla ili kuwapa morali mshinde mechi na Medeama, ni mechi muhimu hii ambayo tunahitaji ushindi wa aina yoyote ile, tunaomba mjitahidi,” alisikika mmoja wa matajiri hao.
Mmoja wa wachezaji wa Yanga waandamizi alisema fedha hizo zilikuwa Sh milioni 10 na waligawana juzi jioni walipofika kambini baada ya mazoezi yao.

Post a Comment

 
Top