RAIS WA SIMBA, AVEVA

UONGOZI wa Simba umesema kuwa hadi hivi sasa haujui hatima ya ujio wa mshambuliaji, Laudit Mavugo.
Mshambuliaji huyo, alitarajiwa kutua Jumatatu wiki hii kwa ajili ya kuanza maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu Bara chini ya Kocha raia wa Cameroon, Joseph Omog lakini hajawasili nchini.
Kinachosikitisha ni kwamba, mwaka jana Simba ilimpa Mavugo Sh milioni 36 kama ada ya usajili lakini timu yake ya Vital’O ikakataa ikisema nayo ilipwe kwani ilikuwa na mkataba na straika huyo.
Kutokana na hali hiyo, Simba ikaona isiwe tabu, ikauchuna hadi Mavugo amalize mkataba wake na sasa straika huyo yupo huru lakini haeleweki na uongozi wa Wekundu wa Msimbazi hauna mawasiliano naye.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Rais wa Simba, Evans Aveva, alisema: “Hatujui hatima ya Mavugo kwani hatumpati kwenye simu, sijui inakuwaje kwani mwanzo tulikuwa tunazungumza vizuri tu.”
MAVUGO

“Tulimalizana naye kila kitu tangu msimu uliopita, akasaini mkataba na fedha tukampa, tunashindwa kuelewa hivi sasa Mavugo hapatikani kwenye simu.
“Tunaamini ameshaitumia fedha ile ya usajili tuliyompa na kuna uwezekano anataka fedha nyingine kwa ajili ya matumizi ya familia yake, angetuambia tumtumie, lakini hapatikani kwenye simu,” alisema Aveva.
Hata hivyo, mara kadhaa Mavugo amekuwa akiwasiliana na Championi Jumamosi huku akisisitiza atumiwe tiketi ya ndege ili aje nchini kuichezea Simba. Taarifa zilizolifikia gazeti hili zinadai kuwa Mavugo huenda akatua wikiendi hii hadi Jumatatu.

Post a Comment

 
Top