MUNGU akiamua huifanya ngumu ionekane nyepesi na laini yaweza kuwa yabisi. Ni yeye aliye juu hubatilisha mipango ya binadamu kwa namna anavyotaka. Ndiyo maana ikasemwa jitihada hazishindi kudura.
Ni kwa ukuu wa Mungu, Bikira Maria, mwanamke ambaye alikuwa hajamjua mwanaume, alibeba mimba ambayo ilimleta duniani Yesu Kristo (Isa bin Mariam).
Hapa ngoja niweke kituo, kisha nikuhoji, ni kipi hasa kinachoweza kukufanya ukimbilie kutoa mimba? Unamjua aliye tumboni mwako amepangwa na Mungu awe nani hapa duniani?
Wewe mwanamke unayenyonga kichanga, ni kwa nini unawahi kukata tamaa mapema na kupitisha hukumu kuwa huwezi kumlea mwanao? Je, unatambua ni sahani gani ambayo Mungu amempa aje nayo hapa duniani?
Umewahi kujiuliza, hivi kama Mark Zuckerberg angetolewa akiwa mimba na mama yake wakati huo, ni nani angeleta mapinduzi ya matumizi ya mtandao kupitia Facebook?
Vipi Bill Gates na Microsoft yake, angewezaje kuyafanya maisha yetu ya kila siku kikazi kuwa rahisi kama mama yake angemnyonga akiwa kichanga?
 
Ni kwa kufikia hoja hiyo ndipo unaweza kuona kuwa wapo watu wengi ambao walimaanishwa kuifanya dunia kama peponi lakini safari yao ilibaki njiani kwa sababu wazazi wao hawakuwapa nafasi ya kuishi.
Ngoja nikwambie ndugu yangu, fursa ya kuishi anaitoa Mungu na ni yeye mwenyewe huyakatisha maisha ya mja wake kwa wakati na namna atakavyo. Juhudi zozote za kukatisha maisha ya mtu ni kuingilia mamlaka ya Muumba!
Mimba inapoingia tumboni, hebu hakikisha unaitunza, maana Mungu ametoa fursa kwa mja wake mwingine kuja duniani. Harakati zako za kwenda kwa madaktari kuichoropoa, kwanza unashindana na mamlaka ya Mungu, pili unapiga teke sahani la almasi.
Je, hupendi kuwa mzazi wa Lionel Messi wa soka? Hutajisikia fahari endapo Steven Curry wa kikapu NBA atakuwa mwanao? Huwezi kufikia hatua hiyo muhimu ya heshima kama hutatii amri ya Mungu, anapoelekeza kiumbe chake ndani ya tumbo lako.
Mwanamke anaweza kutoa mimba kadhaa, kumbe hizo ndizo za wanasayansi wengine kama Neil Armstrong na Buzz Aldrin, waliotangulia kufika mwezini na kufanya ugunduzi mkubwa.
Ungependa mwanao awe mgunduzi wa kihistoria kama Thomas Edison, aliyetengeneza kwa mara ya kwanza taa za umeme, vifaa vya kurekodia sauti na kamera za video, lakini wakati watoto wenye akili kubwa umewanyima fursa ya kuishi.
Lea mimba kwa unyenyekevu wa hali ya juu ikiwa unatamani kuwa na watoto wenye sifa bora kama The Wright brothers, yaani Orville na Wilbur Wright, waliotengeneza na kurusha ndege kwa mara ya kwanza, hivyo kuwa waanzilishi wa usafiri huo wa anga.
Amini kuwa Mungu anapoleta kiumbe chake, anakuwa analeta na sahani yake. Usiogope changamoto za maisha. Endapo utazivumilia si ajabu ukamleta duniani Nikola Tesla, aliyegundua mfumo wa kisasa wa umeme au mwanasayansi Marie Curie ambaye ni mwanamke wa kwanza duniani kutunukiwa Tuzo ya Nobel.
Kuja kuitwa mama wa mfalme, zipo gharama ambazo hutakiwi kuzikimbia. Nyingine ndiyo kama hizo kwamba uwe tayari kubeba mimba katika kipindi ambacho unaona kabisa maisha yako ni magumu.
Mungu ana kawaida ya kuruhusu majaribu yakufike ili yakikuzidi nguvu upotoke. Na mpotokaji anakuwa amechagua njia ya Shetani. Mungu huwapa akili nzuri waja wake pamoja na utashi unaojitosheleza. Unapokosea kwa sababu yoyote ile, maana yake umeshindwa kutumia akili yako ipasavyo.
Muhimu kuzingatia ni kuwa unapopotoka, unakuwa umeshika njia ya Shetani. Mungu aliyekuumba hutaka ubaki kwenye mstari wake hata unapokuwa kwenye wakati mgumu kiasi gani. Muelekee yeye nyakati zote, kuwa na imani isiyoyumba.
Ni kwa imani yako, ndipo unaweza kumleta duniani, Sandford Fleming ambye ni mgunduzi wa majira, mwanzilishi wa stempu za barua, vilevile kiungo muhimu wa uwekwaji wa njia za reli duniani. Usitoe mimba, pengine ukawa mama wa rais au waziri mkuu.
 
CRISTIANO RONALDO ANGETOLEWA AKIWA MIMBA
Dolores Aveiro ni mama wa staa wa soka duniani, Cristiano Ronaldo, anaitwa mama wa stadi huyo wa mpira wa miguu kwa kudura za Mungu. Matunda anayokula ku[itia mwanaye hakika hakuyastahili. Maana anakula raha alizojaribu kuzihujumu.
Kama mipango ya binadamu peke yake ingekuwa inatosha kutimiza mambo na maazimio, Dolores asingeweza kuwa mwanamke maarufu duniani. Asingeitwa mama wa kijana gwiji wa soka duniani, anayeichezea Klabu ya Real Madrid na Timu ya Taifa ya Ureno.
Dolores hakumtaka Ronaldo wakati ikiwa mimba lakini sasa hivi anatamba huku na huko kwamba yeye ndiye mama mzaa nyota. Mungu alimlinda Ronaldo.
Mama huyo, alikusudia hasa kukatisha maisha ya Ronaldo akiwa bado mimba, kwani hata madaktari walipomshauri asifanye hivyo, alitumia mpaka njia za kienyeji.
MAMA RONALDO ANAKIRI
Dolores ameandika kitabu na kukiita kwa Lugha ya Kireno, Mae Coragem (Mother Courage), maana yake ikiwa ni Ujasiri wa Mama. Ndani ya kitabu hicho Dolores anasema: “Nililenga kutoa mimba ya Ronaldo. Nilitumia njia nyingi bila mafanikio.”
Anaongeza: “Madaktari waligoma kunisaidia kutoa mimba, uamuzi uliofuata baada ya hapo ikawa ni kunywa pombe kali ili kutoa mimba. Lakini sikupata matokeo niliyohitaji.
“Nilitumia kila njia nikashindwa. Sikutaka kumzaa Ronaldo. Sikujua kama atakuja kuwa huyu anayenifanya nijivunie kuwa mama.”
RONALDO AMRUDI MAMA YAKE
Ronaldo anajua hila za mama yake, na siku moja alimrudi, akamwambia: “Mama angalia, ulitaka kunitoa nikiwa mimba na sasa mimi ndiye kinara wa nyumba yetu. Unanitegemea na familia yetu yote inanitazama mimi.
“Tazama jinsi ambavyo dunia inanitazama. Naitwa mchezaji mkubwa duniani. Kila klabu kubwa ya soka duniani ingependa kupata huduma yangu. Unadhani hii ni fahari yangu peke yangu? Inakuhusu na wewe mama yangu. Unapaswa kujivunia sana kuwa na mtoto kama mimi.
“Hata hivyo, usingenipata kama ungefanikiwa. Unaweza kuona somo unaloweza kutoa kwa wanawake wengine kuhakikisha wanatunza mimba na kuwalea watoto wao ili waje kujivunia uwepo wao. Pengine wakawa watoto wenye umashuhuri mkubwa duniani.”
Mume wa Dolores, Dinis Averio ambaye ni baba wa Ronaldo, alishatangulia mbele za haki kwa maradhi ya kuharibika kwa ini, ikiwa ni matokeo ya kuathirika na unywaji pombe kupita kiasi.
Hata hivyo, Ronaldo aliijua siri hiyo tangu akiwa mdogo lakini amekuwa akiitunza bila kuitamka popote mpaka pale mama yake alipoamua kuvunja ukimya kwa kuandika kitabu.
 
NINI SHABAHA YA KUANDIKA KITABU?
Kwa mujibu wa Dolares, shabaha yake ni kuwafanya wanawake wengine waone matokeo yake ili wajifunze kwamba unaweza kutoa mimba na kujidanganya kuwa ni salama kumbe umepoteza mkombozi.
“Ningefanikiwa kumtoa Cristiano akiwa mimba, maana yake nisingekuwa mama mwenye thamani kubwa kama nilivyo sasa. Nilikubali kumwacha Cristiano akue tumboni kwangu baada ya kushindwa kumtoa. Nilisema basi tu acha nizae lakini siyo kwa mapenzi yangu.
“Wakati mwingine mpaka huwa nashangaa kila nikikumbuka nilivyokuwa napigania kuitoa mimba ambayo ndiyo imemleta Cristiano duniani. Nikimtazama Cristiano alivyo mkubwa na anavyowika, najiona kabisa kuwa nilitaka kufanya jambo baya na nilikaribia kukatisha maisha ya nyota ya dunia.
“Ananisuta lakini najivunia, maana simuoni mama ambaye asingependa Cristiano awe mtoto wake. Tumboni kwangu ameishi, nilimzaa na kumlea mimi mwenyewe. Ndiyo maana nasema ananisuta lakini najiona mama mwenye fahari kubwa kupitia mwanangu Cristiano,” anasema Dolares.
Anaendelea: “Ona sasa, nimeandika kitabu na kuuza nakala nyingi kwa sababu nimemzungumzia mtoto wangu ambaye ni maarufu sana duniani. Nimepata mafanikio makubwa, nimeingiza fedha nyingi. Nafaidika sana kupitia kuwa mama wa Cristiano.
“Upande mwingine, mimi sina wasiwasi juu ya maisha yangu. Cristiano ananiwezesha kwa kila ninachohitaji. Nikipita barabarani naheshimika. Serikali ya Ureno inaniheshimu. Nikiwa Hispania au popote, hata Uingereza naheshimika.
“Nafahamika mimi ni mama wa Cristiano. Ni faida kubwa sana hii. Daima najivunia kuwa mama wa Cristiano. Nampenda sana Cristiano, namshukuru Mungu kwa kuzuia mpango wangu kutoa mimba yake.”
ANAFAIDI UTAJIRI WA MWANAYE
Kwa sasa Ronaldo anashikilia rekodi ya kuwa mmoja wa wanamichezo wanaoingiza fedha nyingi sana kupitia mshahara na mikataba ya matangazo.
Anatumia gari apendalo na anaishi kwa ufahari mkubwa. Hayo ndiyo matokeo ya Mungu kumlinda Ronaldo mpaka kufikia mafanikio yaliyopo kwa sasa. Na hiyo ni sawa tu na ile bahati ya mtende kuotea jangwani.
WAPO WENYE JUHUDI KUBWA ZA KUUA
Mtu anafanya jaribio la kwanza, mimba haitoki, anarudia tena na tena. Hiyo ni dhamira ya hali ya juu.
Mwingine anafikisha mimba 10 mpaka 20, zote katoa. Kila mwaka anaweka rekodi ya kuchoropoa tatu mpaka nne.
Unaweza kujiuliza kuna nini ambacho mtu anakuwa anakitafuta. Hawezi kuwaza ni wanasayansi wangapi, idadi gani ya wachumi, wanasiasa wakombozi wa nchi, madaktari wenye karama kubwa, waandishi wamulika nchi na kadhalika.
Unakuta mtu anafanya majaribio yote hayo, kisha analaumu kuwa katika uzao wake hajapata mtu mwenye kipaji maalum.
Kila mwanamke atambue kuwa ndani ya tumbo lake kuna tunu kubwa mno. Ni jukumu lake kuitunza. Njia pekee ya utunzaji wa tunu hiyo ni kukilinda kiumbe kinachoingia ndani yake. Zingatia uaminifu!
Kwa mfano mmoja tu wa mama yake Ronaldo, tafakari ni idadi gani ya akina Ronaldo wanapotea? Ndiyo sababu mimi huwa nawaambia watu kuwa Mtanzania aliyetakiwa kuchukua tuzo ya Mchezaji Bora wa Dunia (ballon d’or) kumzidi Messi, pengine alitolewa akiwa mimba au alinyongwa akiwa kichanga.
Mwanamke Mtanzania tishio wa tenisi duniani, mwenye viwango kuliko Serena William, inawezekana naye alinyimwa fursa ya kuishi na wazazi wake, kwa ama kutolewa akiwa mimba au alinyongwa akiwa kichanga au hata alitupwa chooni.
Chukua hii; Kila siku kataa kuupofusha ubongo wako kwa sababu ya upeo wa mboni zako. Kila uamuzi unaofanya hakikisha unatazama juu na mbali kabisa. Changamoto za leo zisikunyime matunda ya kesho.
Hebu nikuombe tuzungumze biashara nzuri na rahisi mno lakini yenye mtaji mkubwa na faida yake inaweza kukufanya ufurahie maisha yako yote. Ukashangaa kila siku unatabasamu, ukitembea unajivuna na watu wanakuheshimu bila shaka.
Kimsingi ni biashara ambayo hata siku moja haiwezi kukupa majuto. Nakuhakikishia pasipokuwa na chembe ya shaka kwamba haitatokea ikakufanya ujilaumu kuifanya.
Naomba uniamini mimi, biashara yenyewe ni uwekezaji kwa mtoto. Wekeza kwa mwanao kisha utaona jinsi maisha yanavyoweza kubadilika kwa kasi.
Weka mipango safi kwa ajili ya mtoto wako na hakikisha unamwita jina zuri kisha umjenge katika misingi iliyo bora.
Usiwe mbinafsi, mpe anachohitaji kama kipo ndani ya uwezo wako. Mwoneshe upendo mpaka yeye mwenyewe akiri kwamba anapendwa.
Watoto ni wakoseaji mara nyingi, siyo yeye ni utoto. Muonye na umsahihishe kwa upendo. Mkaripie na umuadhibu kwa upendo.
Kuwa mtu wa shukurani kila siku. Usimkufuru Mungu. Amini kuwa kwa Muumba kuna neema nyingi nje ya matarajio pamoja na maombi yako. Tambua kwamba aliyekuumba anakupenda kuliko unavyojipenda wewe mwenyewe.
Tukubaliane sasa; Endapo utapata mimba, furahi na useme kuwa hayo ni mafanikio. Usithubutu kusema kuwa imekuja kinyume na matarajio.
Pengine mimba unayosema imekuja kinyume na mipango, ndiye zawadi ya ukombozi. Ipokee na uithamini. Nakuhakikishia hutajuta.
Kuna siku ngumu inakuja, ambayo wengi watashindwa kujibu maswali ya Muumba na malaika wake. Siku tamu kwa watu wema na ngumu kwa waovu. Inaitwa siku ya mwisho.
Siku hiyo hukumu itatolewa. Na ikifika, wapo marais, wanasiasa wakubwa, wanasayansi waliomaanishwa kuja kuikomboa dunia, viongozi wa kidini na kadhalika, watasimamishwa kwenye uwanja wa hukumu, kisha kutangazwa kuwa ni mashujaa walionyimwa fursa ya kuishi na wazazi wao.
Tuendelee kukumbushana. Tunaweza kujenga kizazi kizuri kwa faida ya leo na kesho. 
mwandishi: Luqman Maloto

Post a Comment

 
Top