NYOTA wa soka jicho la Watanzania, Mbwana Ally Samatta, ameendelea kuiweka hai furaha ya Watanzania.
Kuanzia tuzo ya
Mwanasoka Bora Afrika kwa wachezaji wa ndani, kusajiliwa barani Ulaya
kwenye timu ya Koninklijke Racing Club Genk (KRC Genk) ya Ubelgiji na
baadaye kuanza vizuri kwa kutikisa nyavu ni mambo yaliyawapa burudani
Watanzania.
Februari 28,
mwaka huu, Samatta alifunga goli muhimu, lililoiwezesha KRC Genk kupata
ushindi wa mabao 3-2 nyumbani dhidi ya vinara Ligi Kuu ya Ubelgiji, Club
Brugge KV.
Mambo mswano kabisa! Kila jema ambalo Samatta analifanya ndivyo anavyowatoa kimasomaso Watanzania.
Watanzania
waliomba na kutarajia na hakika imekuwa kweli. Hongera sana Mbwana kwa
kutwaa tuzo ya Mwanasoka Bora Afrika kwa wachezaji wa ndani ya Bara la
Afrika kisha kupata matunda mema Ulaya.
Tuzo ya Samatta
na mafanikio yake kwa jumla, yana maana kubwa kwa mtu yeyote
anayehitaji mafanikio. Neno moja tu lina uzito wa kutosha kutoa tafsiri
pana ya hatua anazopita mchezaji huyo aliyetokezea Mbagala, Dar es
Salaam.
Na neno lenyewe
ni nyakati. Naam! Samatta alizitafuta na sasa amefikia wakati wake,
ilikuwa lazima ashinde tuzo kisha kupata mafanikio Ulaya ambayo ameanza
nayo kwa sababu huu ni wakati wake.
Samatta ilikuwa vigumu mno kwake kushinda tuzo mwaka jana, na kutikisa Ulaya hapo kabla kwa sababu haukuwa wakati wake.
Mwaka jana na mingine michache iliyopita ilikuwa awamu yake ya kutikisa kwenye Klabu ya TP Mazembe ya DRC.
Mwakani anaweza
kushinda tuzo nyingine kubwa zaidi, yaani ile ya Mchezaji Bora wa
Afrika (tuzo ya jumla) kama itakuwa ni wakati wake. Na anaweza kushinda
tena na tena!
![]() |
chuji |
Mafanikio ya Samatta yanamaanisha nini? Jawabu moja, attitude! Hicho ni Kiingereza, Kiswahili tunaita hulka.
Wapo wachezaji
wengi wamepita nchini, walikuwa na vipaji pamoja na viwango vikubwa
kuliko Mbwana lakini hawakuweza kufika popote kwa sababu ya hulka
(attitude).
Hulka bora
ndiyo nidhamu. Wapo wachezaji wa soka walimaanishwa kutikisa nchini na
duniani kwa jumla wakitokea Tanzania, lakini hulka zao ziliwaponza.
Madini yao ya ndani ya uwanja, yameishia mchangani! Maskini yao!
Lazima kuheshimu hulka ili kutumia wakati wako vizuri. Na hii ni kwa kila fani, siyo katika soka peke yake.
Mwanamuziki
Diamond Platnumz au Nasibu Abdul Juma, anatikisa Afrika kwa sasa
akitokea Tanzania, ni kwa sababu hulka yake ilimfanya aufanye wakati wa
sasa kuwa mwafaka kwake.
Yeyote anayejituma, na akiwa na hulka njema, anaweza kufanya maajabu yenye kugeuza chupa kuwa almasi.
Na mafanikio ya
Samatta na Diamond, yawe fundisho kwa kila mmoja kutambua wakati wake
na kuutumia vizuri kufika mbali na kupata mafanikio stahiki.
Wapo wengi
hawakutumia vizuri nyakati zao. Alikuwepo fundi Haruna Moshi ‘Boban’,
akasajiliwa Gefle IF ya Sweden mwaka 2010. Akatarajiwa kufika mbali.
Haikuwa hivyo, alirejea nchini kwa kususa na alipofika Bongo, hakuwa
Boban yule tena!
Ameishia wapi
Athuman Idd ‘Chuji’? Alikuwa kiungo aliyekamilika kiukweliukweli.
Alihitaji nidhamu tu, yaani kuwa na hulka kama za Samatta, hakika dunia
nzima ingemwelewa.
Jaribu kuwaza
kipaji cha Boban, halafu angeongezewa na nidhamu ya Samatta. Jibu
unaweza ukawa unalo ni wapi ambapo leo hii angekuwa.
![]() |
boban |
Mlete Chuji
kwenye mawazo yako, kifikirie kile kiwango chake, hapohapo itoshe kukupa
jawabu kuwa wacheza soka wa Tanzania walitakiwa kuwa wenyeji wa Ulaya
miaka mingi nyuma ila wamekuwa wakiponzwa na hulka zao.
Shika muongozo
kuwa juhudi na nidhamu huvuta bahati, kisha bahati ndiyo itakufanya
ufike kwenye kipindi chako cha mafanikio. Kwa hiyo hulka inapaswa kuanza
kabla ya vyote.
Muongozo ni
wewe kujituma na utakapofika kwenye wakati wako, hakikisha unautumia
vizuri ili utakapopita, watu waseme “alikuwepo fulani bwana!”
Pambana kwenye
eneo lako ili utengeneze wakati wako mzuri. Utakuwa mwenye kupendwa na
kuheshimika sana kama utafikia wakati wako na kufanya kile
kinachohitajika.
Kila mwanasoka,
hususan wale chipukizi, wanalo la kujifunza kupitia kwa Samatta,
vilevile wajiongeze kutoka walipokwama akina Boban, Chuji na wengine
ambao walikwama njiani kutokana na hulka zao.
mwandishi: Luqman Maloto
Post a Comment