SUALA la beki
Hassan Kessy limeingia katika sura mpya baada ya uongozi wa Simba kupeleka
barua kwenye Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Barua hiyo ya Simba, inaonyesha kuwa klabu
hiyo inataka kulipwa dola 60,000 (zaidi ya Sh milioni 126), ili Kessy aanze
kuichezea Yanga.
Habari za uhakika ambazo Championi Jumatano
imezipata kuwa barua hiyo tayari imewasilishwa TFF na Yanga taarifa wanazo.
Simba wamepeleka barua hiyo TFF wakitaka
fedha hizo kwa kuwa Kessy alivunja mkataba.
Mkataba wa Kessy na Simba unaonyesha
atakayevunja anatakiwa kulipa fedha hizo.
“Barua ambayo Simba wameipeleka TFF
inaonyesha kwamba Mei 25, Kessy alipanda jukwaani akiwa na jezi ya Yanga na
baadaye akashangilia ubingwa na wachezaji wa Yanga wakati huo akiwa na mkataba
na Simba ambao ulipaswa kuisha Juni15,” kilieleza chanzo.
“Hiyo inatosha kuonyesha alivunja mkataba,
lakini Simba wameanzisha kitu kingine na kupeleka TFF, kwamba Kessy alisafiri
na Yanga kwa siri kwenda Misri wakati ilipokwenda kucheza na Al Ahly wakati
akijua ana mkataba na Simba.
“Msisitizo wa Simba, wanasema pia wakati
kibali cha Kessy kinatoka pia alikuwa Uturuki na Yanga na baadaye alikwenda
Algeria ambalo ni kosa jingine na hili Yanga wanalijua kwa kuwa barua iko TFF.”
Wakati chanzo hicho kinaeleza hilo, taarifa
nyingine zimeeleza kwamba Sputanza imeanza kulishughulikia suala hilo ikitaka
Simba imuachie Kessy acheze Yanga kwa kuwa tayari mkataba wake na Simba uliisha
Juni 15.
Alipoulizwa Mkuu wa Kitengo cha Habari na
Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro kuzungumzia hilo alisema kuwa: “Kama Yanga
hatuna taarifa hizo za kutaka fedha hizo, lakini sisi tulimsajili Kessy kama
mchezaji huru, sasa linavyokuja suala hilo tunashindwa kuelewa, acha tusubirie
barua hiyo itufikie ndiyo tutoe tamko letu.
Naye Meneja wa mchezaji huyo, Athumani Tippo
alisema: “Suala nisingependa kulizungumzia kwa sasa, kwa sababu mimi kama
meneja wa mchezaji nilifuata sheria zote za usajili ikiwemo kufanya mazungumzo
na Yanga ndani kipindi muafaka cha miezi sita ambacho Kessy mkataba wake ulikuwa unamalizika na baadaye
kusaini mkataba, sasa hizo fedha wanazozitaka ni za nini?
Kessy mwenyewe alisema: “Ujue ninashindwa
kuelewa, sasa hizo fedha wanazozihitaji Simba za nini jamani? Mimi mbona
nilisaini Yanga kama mchezaji huru baada ya mkataba wangu kumalizika.
“Mimi nisingependa malumbano katika kipindi
hiki na Simba, ninaomba suala hili limalizike kwa amani bila ya kugombana kwa
sababu katika maisha kuna leo na kesho na wakumbuke mimi mchezaji maisha yangu
yanategemea soka,”alisema Kessy.
Post a Comment