IMEFAHAMIKA kuwa, baada ya Yanga
kuchelewesha kuwasilisha majina ya wachezaji wao watakaowatumia kwa msimu ujao
wa Ligi Kuu Bara, timu hiyo italazimika kulipa faini ya dola 500 kwa kila
mchezaji ambazo ni sawa na shilingi milioni moja.
Kwa mujibu wa taarifa za ndani kutoka
katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Yanga imewasilisha majina ya
wachezaji 28 kwa ajili ya msimu ujao, lakini ilikuwa nje ya muda uliopangwa.
Hivyo jumla watatakiwa kutoa zaidi ya Sh milioni 28 kama faini.
Agosti 6, mwaka huu usajili wa
wachezaji kwa timu za Ligi Kuu Bara, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la
Pili ulifungwa, ambapo Yanga na Coastal Union hazikuwasilisha kwa wakati majina
ya wachezaji wao ndani ya TFF, jambo ambalo limezua mjadala.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya
TFF, zimeeleza ni wazi Yanga na Coastal zitapigwa faini kwani tayari
zimewasilisha barua ya utetezi kama walivyotakiwa kufanya kueleza kwa nini
zimechelewesha majina ya wachezaji wao.
“Baada ya kuwataka walete barua za utetezi
wao, tumezipokea, hivyo kinachofuata hapo ni lazima watapigwa faini na si
kingine.
“Hapa Yanga imewasilisha majina ya
wachezaji wao 28, hivyo watatakiwa kulipa dola 500 kwa kila mchezaji, sasa hapo
ukifanya hesabu kwa jumla nadhani utapata hiyo faini ni kiasi gani cha fedha,”
alisema mtoa taarifa hiyo.
Championi lilimtafuta Katibu wa TFF,
Selestine Mwesigwa kuzungumzia hilo, simu yake iliita bila ya kupokelewa,
lakini Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas alisema ni wazi timu hizo zitapigwa
faini kutokana na kanuni zilivyo japo hakufafanua ni kiasi gani.


Post a Comment