WINGA wa zamani wa Yanga, Mrisho Ngassa, anayekipiga Fanja ya nchini Oman yupo Bongo kwa sasa na inadaiwa kuwa amekuja kwa ajili ya kufanya mazungumzo na uongozi wa Yanga ili kujaribu kuushawishi uweze kumsajili.

Hata hivyo, habari za kuaminika kutoka ndani ya Yanga zimedai kuwa nyota huyo ambaye pia amewahi kuzitumikia Kagera Sugar, Simba, Azam na FreeState ya Afrika Kusini, ameondoka kwa kudanganya katika timu yake ya Fanja na kuja hapa nchini ili kufanikisha dili hilo.

Mara kadhaa Ngassa amekuwa akihusishwa kutaka kurejea kikosini humo tangu aachane nacho kwenda FreeState baada ya msimu wa 2014/15.

“Ni kweli Ngassa yupo hapa nchini na hivi karibuni alikutana na baadhi ya viongozi wetu na kuzungumza nao akiwaambia kuwa anataka kurejea Yanga.

“Katika timu yake hiyo ya Fanja aliaga kuwa ana matatizo ya kifamilia, hivyo anatakiwa akayamalize, nao bila ya kujua wakamruhusu kumbe lengo lake kubwa ni kuja kuushawishi uongozi ili uweze kumsajili katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili.

“Hata hivyo, mpaka sasa viongozi wametofautiana kuhusiana na suala hilo ambapo wapo wanaotaka na wengi hawataki wanadai kuwa kwa sasa hana sifa za kuitumikia Yanga,” kilisema chanzo hicho cha habari.

Alipotafutwa Ngassa kuhusiana na ishu hiyo, alikiri kuwepo nchini kutokana na matatizo ya kifamilia yaliyosababisha aje ili kuyatatua.
 “Mkataba wangu haunibani kujiunga na klabu yoyote baada ya miezi mitatu, muhimu ni utaratibu wa kiusajili kufuatwa,” alisema na kufunguka zaidi kuhusu Yanga:

“Yanga ni timu yangu ya zamani na sioni sababu ya kutorejea kutokana na mafanikio niliyoyapata nikiwa pale.”

Ngassa alirejea juzi Jumanne usiku akitokea Mwanza alipokwenda kutatua matatizo ya kifamilia.

Post a Comment

 
Top