KOCHA Mkuu wa JKT Ruvu, Hamsini Malale, amesema atahakikisha anaisimamisha Simba kwa kuibuka na ushindi katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, utakaochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Simba wameanza msimu mpya kwa kishindo baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Ndanda FC, katika mchezo uliochezwa juzi, Uwanja wa Taifa.
Akizungumza na BINGWA jana, Malale  alisema pamoja na Simba kuibuka na ushindi huo, lakini washambuliaji wao tegemeo, Ibrahim Ajib na Laudit Mavugo hawatapata nafasi ya kusumbua mabeki wake, kutokana na majukumu aliyowapa.
Malale alisema  Simba wasitegemee mteremko kutoka kwao, kwani wamejiandaa katika kuhakikisha wanaondoka na pointi tatu ili waweze kuanza msimu  kwa matokeo mazuri.

Alisema wataendeleza ushindi kwa Simba baada ya kuwafunga mabao 2-1 katika mchezo wa mwisho wa msimu uliopita.
Malale alisema anaendelea kuboresha kikosi chake ili kiweze kucheza soka ya ushindani, ili waweze kuibuka na ushindi.
Alisema ili waweze kuleta mabadiliko na matokeo mazuri, wachezaji wao wamekuwa wakifanya mazoezi makali ili kuwajengea ufiti.
“Maandalizi yapo vizuri, tutahakikisha wachezaji wanacheza kwa nidhamu na utulivu ili kuweza kupata ushindi,” alisema Malale.

Post a Comment

 
Top