HUU ni mwaka wa neema Simba SC. Huu ndio ukweli kwani baada ya kukubali kubadili mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo ambao utaruhusu bilionea, Mohamed Dewji maarufu kama Mo kuwekeza fedha nyingi, klabu hiyo sasa iko mbioni kupata dili lenye pesa nyingi za udhamini.

Katika mfumo mpya, Mo atawekeza kiasi cha Sh bilioni 20 kwa kununua hisa 51 za klabu hiyo huku hisa nyingine zikinunuliwa na wadau wengine wakiwemo wanachama wa klabu hiyo kongwe ya jijini Dar es Salaam.

Mbali na uwekezaji huo, klabu hiyo sasa ipo katika hatua za mwisho za mazungumzo ya udhamini na Benki ya NMB hasa baada ya kumalizika kwa mkataba wa udhamini na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) ambayo ilikuwa ikiidhamini klabu hiyo kupitia bia yake ya Kilimanjaro.

Mwenyekiti wa Kamati ya usajili ya klabu hiyo, Zacharia Hanspope, aliliambia BINGWA kuwa klabu hiyo ipo kwenye mipango kabambe ya kupata wadhamini mbalimbali ili kuhakikisha wanatunisha mfuko wa klabu hiyo na moja ya wadhamini hao ni NMB.

“Mpaka sasa NMB ndio wameonyesha nia ya kutudhamini, mazungumzo yako katika hatua nzuri sana lakini pia bado milango iko wazi kwa ajili ya makampuni na mashirika mengine,” alisema.

Hata hivyo, Hanspope alikataa kuweka wazi thamani ya mkataba huo, lakini alisema kwamba utakuwa ni moja ya mikataba minono itayoinufaisha Simba na kuipa fedha za uhakika kulingana na thamani na ukubwa wa klabu hiyo.

NMB ambayo inaidhamini Azam kwa miaka miwili ambapo klabu hiyo ya Chamazi jijini Dar es Salaam, imenufaika kutokana na udhamini huo ambao kila mwaka ilielezwa walipata milioni 500 kutokana na udhamini huo.

Azam ilikuwa ikivaa jezi zenye nembo ya NMB kifuani kuanzia mazoezini hadi kwenye mechi zote walizokuwa wanashiriki za Ligi Kuu na zile za mashindano ya kimataifa.

Awali Simba iliwahi kuingia mkataba na benki hiyo mwaka 2004, lakini baadaye mkataba huo ulivunjika kabla ya kumalizika kutokana na kukiukwa kwa makubaliano ya mkataba huo.


Pia NMB iliwahi kuidhamini timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars kati ya mwaka 2007 na 2010 ikiwa chini ya kocha Mbrazil, Marcio Maximo.

Post a Comment

 
Top