LICHA ya kuonekana kama vile Simba ina uhitaji wa kipa mwingine ili kuwa mbadala wa kipa namba moja wa sasa, Vincent Angban, Wekundu hao wa Msimbazi wamesema kwa sasa hawafikirii jambo hilo.

Simba ina makipa watatu, Angban ambaye anaonekana kuwa tayari amejihakikishia nafasi kikosi cha kwanza, pamoja na Peter Manyika na Denis Richard ambao bado wanachipukia.

Hivi karibuni kabla usajili wa wachezaji wa ndani haujafungwa, iliripotiwa klabu hiyo kumtaka kipa wa Azam, Mwadini Ali ajiunge na timu hiyo kwa mkopo, lakini dili hilo likakwama.

Kocha wa Makipa wa Simba, Adam Abdallah ‘Meja’, amesema Angban anatosha kuivusha Simba kutoka hapo ilipo na kwenda mbele zaidi, hivyo kwa sasa hawafikirii kuanza kuumiza kichwa kusaka kipa mwingine wa kiwango cha juu zaidi yake.

“Tunao makipa watatu na wote wanaonyesha viwango vya hali ya juu tukiwa mazoezini, yule anayeonekana kuwazidi wenzake ndiye anayepata nafasi kwenye mechi.

“Ukiangalia ligi ndiyo kwanza imeanza na Angban ameanza vizuri kwa kudaka akianzia zile mechi za maandalizi ya msimu, lakini hiyo haiwezi kumfanya kujihakikishia nafasi kikosi cha kwanza.

“Ikitokea siku Denis na Manyika wamefanya vizuri mazoezini, basi watapata nafasi ya kucheza huku Angban akikaa benchi au hata jukwaani,” alisema Meja.


Post a Comment

 
Top