MSHAMBULIAJI wa Simba raia wa Ivory Coast, Fredrick Blagnon,  ameanza kuzua hofu kwa mahasimu wa jadi wa klabu hiyo, Yanga, baada ya kuonyesha uwezo wa hali ya juu katika mechi alizocheza Uwanja wa Taifa, ikiwemo mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Ndanda.

Simba walishinda mabao 3-1, huku Blagnon akifunga bao la pili kwa kichwa na kuanza kuzamisha jahazi la Ndanda ambao walikuwa na matumaini ya kuibuka na sare kwenye mchezo huo.

Blagon, aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Ibrahim Ajib, alibadilisha sura ya mchezo huo kwa Simba ambayo ilipanga vyema mashambulizi yake na hatimaye kupata bao la pili na la tatu.

Kutokana na uwezo ulioonyeshwa na Blagon, watani wao wa jadi, Yanga, wameanza kutishika huku uwezo wa mchezaji huyo ukiibua mjadala mkubwa kwa mashabiki wa Yanga kuelekea katika mchezo wao wa ligi Oktoba mosi, mwaka huu.

Habari zilizopatikana jana zilieleza kwamba benchi la ufundi la Yanga, linaloongozwa na Hans van der Pluijm, limeanza kukuna kichwa jinsi ya kukabiliana na washambuliaji wa Simba, akiwemo Blagon, ambaye ameonekana kuwa na uwezo mzuri.

Benchi la ufundi la Yanga sasa linajipanga pamoja na mambo mengine, kuhakikisha viungo wao, Thaban Kamusoko na Haruna Niyonzima wanakuwa na mbinu za kukabiliana na Blagon, ambaye licha ya kwamba anacheza nafasi ya ushambuliaji, lakini ameonekana kuwa ni mtu anayeweza kusumbua pia nafasi ya kiungo.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa Simba,  Patrick Kahemele, amesema Blagnon atawakimbiza mabeki na viongo wa  timu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara  kutokana na uwezo wake uwanjani.

Kahemele alisema Blagnon msimu huu anaweza kuwa mfungaji bora kutokana na uwezo mkubwa wa kupachika mabao kwa kutumia kichwa na miguu.

“Huyu jamaa ni hatari sana, subiri uje uone wapinzani watakavyolizwa na mabao yake, tena nakwambia atakuwa mfungaji bora msimu huu, kutokana ana kila sifa ya kuwa mshambuliaji,”  alisema Kahemele.

Blagon, pamoja na kwamba atatumika kama mshambuliaji, lakini yeye ni kiungo mchezeshaji, hivyo Kocha wa Simba, Joseph Omog, anaweza kumtumia katika nafasi yoyote kati ya hizo na katika mechi ngumu kama ya Yanga huenda akamtumia katika nafasi ya kiungo.

Post a Comment

 
Top