KAMA ulidhani Yanga watapoteana Ligi Kuu baada ya kupata matokeo mabaya Kombe la Shirikisho Afrika, imekula kwako kwani Wanajangwani hao wanapewa nafasi kubwa ya kutetea ubingwa wao.

Yanga wameyaaga mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kushika nafasi ya mwisho kwenye kundi lao na sasa wanarudi Ligi Kuu wakiwa na hasira.

Kutokana na kucheza muda mrefu baadhi ya mashabiki na wapinzani wa Yanga wanadhani kuwa wachezaji wa Yanga hawatakuwa kwenye ubora wao, lakini wachambuzi wa soka wanasema kuwa hiyo imezidi kuwapa uzoefu.

Kocha na mchambuzi wa soka nchini, Kenny Mwaisabula ‘Mzazi’, amesema kuwa uzoefu walioupata Yanga katika michuano ya kimataifa utawasaidia sana kwenye ligi  katika harakati za kutetea taji lao msimu huu.

Mwaisabula alisema kuwa Yanga wamecheza mechi nyingi na wamekaa pamoja kwa muda mrefu jambo ambalo litawafanya wawe kwenye ubora zaidi wanaporejea kwenye Ligi Kuu kuliko watu wanaavyodhania.

“Ukiangalia timu zinazoshiriki kwenye ligi, nyingi zimebadili kikosi, mabenchi ya ufundi hiyo itachukua muda kidogo kucheza kitimu kwani hawajazoeana sana, tofauti na ilivyo kwa Yanga kwani hata wale wapya waliowasajili hivi karibuni tayari wameshacheza mechi pamoja na hivyo kila mmoja kumjua mwenzake,” alisema.

Kwa upande wa mchambuzi wa soka wa kituo cha Efm na gazeti hili, Oscar Oscar, amesema kuwa Yanga wana nafasi kubwa ya kutetea taji lao msimu huu licha ya kwamba kutakuwa na upinzani mkali kutoka kwa watani zao Simba na pengine Azam.

“Kulingana na vikosi vilivyo msimu huu, Simba ndio wanaoweza kuwasumbua kulingana na usajili wao lakini pia hivi sasa hawana tatizo la ukata lililokuwa likiwatesa kwa muda mrefu hasa baada ya ujio wa mfanyabiashara, Mohamed Dewji ‘Mo’ ambaye ameonyesha nia ya kuwekeza kwa Wekundu hao wa Msimbazi.

“Mbali na hilo, Yanga wana nafasi ya kutetea taji lao kwani kwa muda mrefu kikosi kipo pamoja na benchi la ufundi ni lile lile jambo ambalo limewaepusha wachezaji  kufanya mambo ambayo yangeweza kuwafanya wasiwe kwenye ubora wao kama vile ulevi, kucheza ndondo na kupata majeraha yasiokuwa na sababu za msingi,” alisema.

Alisema kuwepo kwao pamoja kunawafanya waendelee kuwa kwenye ubora wao na kucheza soka la ushindani, lakini hilo litawezekana iwapo kocha Hans van de Pluijm, atakuwa tayari kuwapumzisha wale wachezaji waliocheza mechi nyingi na kuonekana kucheza na hivyo kutoa nafasi kwa waliokuwa nje kwa muda mrefu.

“Iwapo kama Pluijm atakubali kuwapumzisha baadhi ya wachezaji wanaoonekana kuchoka kutokana na kukosa muda wa kupumzika na kuwatumia wengine, ataweza kuwa na kikosi cha ushindani lakini akiendelea na yale maamuzi yake ya kuwang’ang’ania wale wale basi tusitegemee ushindani mkubwa kutoka Yanga kwani wachezaji hivi sasa ni wazi wamechoka na wanahitaji muda wa kupumzika, ingawa Yanga wana kikosi kipana zaidi na kilichojaa wachezaji mahiri,” alisema.

Aidha, kocha Fred Minziro, alisema wanatagemea Yanga itakuwa imepata uzoefu kutokana na kuwa mashindano waliyoshiriki ni makubwa kuliko Ligi Kuu Tanzania Bara.

Alisema Yanga wataingia kwenye ligi wakiwa na nguvu mpya hasa ukizingatia wametoka kupambana na timu ngumu ukilinganisha na zile zinazoshiriki ligi.

“Kwa maoni yangu watakuja wakiwa vizuri zaidi lakini ushindani utakuwepo licha ya uzoefu walioupata, uchovu utawaathiri kwa sababu wamecheza kwa muda mrefu bila kupumzika na wakirudi wanaingia moja kwa moja kwenye ligi,” alisema Minziro.

Kwa upande wake kocha wa timu ya Taifa, Charles Mkwasa, alisema Yanga licha ya kutolewa katika hatua hiyo wamejifunza vitu vingi vitakavyowasaidia kwenye mechi za Ligi Kuu.

Alisema mashindano waliyoshiriki  yamekuwa katika ushindani na timu kubwa hivyo wataingia kwenye ligi wakiwa wanajiamini zaidi.

Hata hivyo, Mkwasa alisema Yanga itakutana na changamoto  za upinzani kutoka kwenye timu watakazokutana nazo katika ligi ambapo kila mmoja atataka kuonyesha uwezo wake.

“Yanga watakutana na vikwazo vya wapinzani ambao watakuwa wanacheza  kwa kujituma zaidi kupata matokeo mazuri  na kutaka kama kuwatoa Yanga nishai ili kudhihirisha ubora wao, kwamba nao wanaweza kukabiliana  hata kama hawajashiriki michuano mikubwa,” alisema Mkwasa.
ChanZO: Bingwa

Post a Comment

 
Top