KATIKA hali ya kushangaza, wachezaji wa Yanga, juzi Jumamosi waligoma kufanya mazoezi ya mwisho kabla ya kusafiri kuelekea DR Congo kwa ajili ya mchezo wao wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya TP Mazembe yaliyokuwa yakiongozwa na kocha mkuu wa timu hiyo, Mholanzi, Hans van Der Pluijm kutokana na madai ya Sh milioni 100 wanazodai zikiwemo za usajili.
Yanga, Ijumaa iliyopita ilifanya mazoezi katika Uwanja wa Uhuru kabla ya juzi Jumamosi kugoma kabisa kuendelea na programu hiyo kufuatia madai hayo wakiushinikiza uongozi uwalipe fedha zao ambazo uliwaahidi hapo awali kutokana na kufanya vizuri msimu uliopita.
Championi ambalo Jumamosi lilifika uwanjani hapo, liliwashuhudia wachezaji hao wakiwa wamekaa na nguo zao za nyumbani tofauti na ilivyozoeleka kabla ya kuamua kutoka uwanjani na kila mmoja kuchukua njia yake huku Pluijm akiendelea kupanga vifaa vya kufanyia mazoezi siku hiyo zikiwemo koni.
Wakati wachezaji wanafanya kikao chao, meneja wa timu hiyo, Hafidh Saleh alikuwa na kikao kingine na kaimu katibu mkuu wa timu hiyo, Baraka Deusdedit ambao nao kwa pamoja walianza kutoka ndani ya eneo la uwanjani kuelekea kwenye basi la timu ikiwemo kutoa vifaa vyote na kuanza kuviweka ndani ya basi huku Pluijm naye akiamua kwenda kwenye gari lake kubadilisha nguo kwa ajili ya kutoka uwanjani hapo.
 Championi lilimfuata meneja wa timu hiyo ambaye hakutaka kuongea chochote zaidi ya kumtupia mpira Deusdedit ambaye alidai ndiye mwenye uwezo wa kuongea kilichotea.
Hata hivyo, kiongozi huyo hakuwa tayari kulitolea ufafanuzi jambo hilo zaidi ya kusikika akilalamika akisema: “Kiukweli hii timu imeshanichosha yaani kila kitu ni shida, wanachama nao hivyohivyo na wachezaji nao wamezua balaa lingine, sijui hata nifanye nini.”
Lakini taarifa za ndani zinasema kuwa wachezaji hao wameamua kugoma wakishinikiza uongozi wa timu hiyo utekeleze ahadi walizoahidiwa.
 “Wachezaji wameamua kugoma kwa sababu wanadai fedha nyingi kutoka kwa uongozi ambazo uliwaahidi hapo awali zikiwemo fedha za kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara, ubingwa wa Kombe la FA, kuwatoa APR katika Ligi ya Mabingwa Afrika na kufuzu hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika.
“Fedha ni nyingi kwani zinafikia milioni 100 kutoka katika mashindano hayo yote, lakini wanaona hakuna kinachoeleweka, kila siku yamekuwa maneno kwani pia wanadai na fedha za usajili wengi walikuwa hawajamaliziwa, kitu ambacho kinawakatisha tamaa na morali ya kucheza, maana hata ishu ya kuchukua ubingwa wa msimu huu sina hakika kama itawezekana,” kilisema chanzo hicho.
Alipotafutwa kwa njia ya simu Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga, kwanza aliipokea vizuri, lakini mwandishi alipojitambulisha, kiongozi huyo akakata simu na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi hakujibu.
Katika hatua nyingine, kikosi cha Yanga jana Jumapili kilisafiri kuelekea DR Congo kikiwa na wachezaji 19, watu saba wa benchi la ufundi, kiongozi mmoja wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na kaimu katibu mkuu wa klabu hiyo.
Timu hiyo imeenda nchini humo kumalizia mchezo wa mwisho wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya TP Mazembe utakaopigwa kesho Jumanne.

Post a Comment

 
Top