mavugo


KOCHA wa Simba, Joseph Omog, amewaweka kitimoto mastraika wake Mrundi, Laudit Mavugo na Ibrahim Ajib na kuwataka kuacha ubinafsi wanapokuwa uwanjani na badala yake wacheze kwa kushirikiana na mwenye kuzingua benchi litamhusu.

Kuelekea kwenye pambano la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya JKT Ruvu litakalochezwa kesho kwenye Uwanja Taifa, Dar es Salaam, Omog ameona awaweke chini mastraika wake hao tegemeo na kuwataka kuacha uchoyo uwanjani na kucheza kwa ajili ya timu na si mafanikio binafsi.

Omog aliwapa onyo hilo mastaa hao wawili wa Simba baada ya kuwatazama kwenye mechi ya kwanza ya Ligi Kuu na zile mbili za kirafiki dhidi ya AFC Leopards na URA na kugundua kuwa kila mmoja amekuwa akicheza kichoyo anapokuwa uwanjani.

Kocha huyo wa zamani wa Azam, alionekana kuchukizwa na tabia ya Mavugo na Ajib kucheza kichoyo wakati timu yake ikiwa inahitaji ushindi kitu ambacho kinaweza kuwaumiza siku za usoni.

Ajib katikati
Akizungumza na BINGWA, Omog alisema amewaweka chini mastraika hao wawili na kuwapa onyo kali huku akisisitiza kuwa mchezaji ambaye ataendelea na tabia hiyo ya uchoyo kumsugulisha benchi au kumtoa uwanjani kama akiwa anacheza.

“Timu kwanza mtu baadaye, hakuna ubinafsi kama mtu anajiona yeye ni mbinafsi aachie ngazi wengine wafanye kazi, hatupo hapa kujionyesha kila mtu anaweza,” alisema Omog.

Alisema kitendo cha mastraika hao wawili kucheza na kunyimana pasi katika mchezo uliopita dhidi ya Ndanda FC kulilipa wakati mgumu benchi la ufundi la timu hiyo katika kipindi chote cha dakika 90 za mchezo huo.

“Tulikuwa tuna uwezo wa kufunga mabao zaidi ya matano siku ile, lakini kwa tabia zao za kunyimana pasi na kucheza kibinafsi kulitupa wakati mgumu sana pamoja na kuwa tulishinda mchezo ule,” alisema Omog.

Aliongeza kusema kuwa Simba msimu huu imedhamiria kufanya kweli ndio maana benchi la ufundi la timu hiyo limeweza kusajili kikosi kipana kilichosheheni lundo la wachezaji wenye vipaji vya hali juu.

“Hakuna Mungu mtu, nina washambuliaji wengi kama Fredrick Blagnon, Danny Lyanga na Ame Ali kwa hiyo atakayeshindwa kwenda na sera zetu aachie ngazi mapema,” alisisitiza Omog.

Simba kesho itashuka katika dimba la Taifa jijini Dar es Salaam kuwavaa maafande wa JKT Ruvu ikiwa ni mchezo wao wa raundi ya pili ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Post a Comment

 
Top