HATIMAYE klabu za Simba na Yanga, zimejikuta katika nafasi ya kujiimarisha zaidi kiuchumi hivyo kuwa na uwezo wa kuvisuka vikosi vyao na kuwa tishio barani Afrika, ikiwa ni matokeo ya mkakati kabambe wa Rais John Magufuli wa kuimarisha uchumi nchini.
Tangu Rais Magufuli alivyoingia madarakani Oktoba mwaka jana, amekuwa akihimiza kwa nguvu zote ukusanyaji wa kodi, lakini pia kudhibiti mianya yote ya rushwa na kila aina ya wizi kama sehemu ya kuimarisha usimamizi wa mali na fedha za Serikali.
Matokeo yake wale waliokuwa wakijipatia fedha kwa njia za mkato na nyinginezo zisizo halali, wamejikuta wakiwa katika hali ngumu, lakini pia mpango huo wa Rais Magufuli ukionekana kuathiri kwa kiasi kikubwa uchumi wa baadhi ya watu kama ilivyo kwa kampuni, mashirika na sekta binafsi kadha wa kadha.
Kutokana na hali hiyo, wafanyabiashara wengi wamekuwa wakiumiza vichwa kuona ni vipi wanaweza kuzinadi bidhaa au huduma zao ili waweze kupata soko litakalowawezesha kuendelea na shughuli zao.
Na baada ya mfanyabiashara, Mohammed Dewji ‘Mo’, kujitokeza kutaka kununua hisa za klabu ya Simba, huku kwa upande wa Yanga akijitokeza bilionea anayetaka kumiliki nembo ya klabu hiyo, makampuni na mashirika kadha wa kadha yameanza kuzigombania klabu hizo ili kuzidhamini ziweze kuzitumia kama ubao wa matangazo ya kunadi bidhaa zao.
Unajua ni vipi? Kwa kuwa klabu hizo zina mashabiki wengi kila kona ya nchi na nje ya Tanzania, wafanyabiashara, makampuni na mashirika mbalimbali yanaamini iwapo watazidhamini, itakuwa ni njia rahisi kupata soko la bidhaa zao kupitia kwa wapenzi wa miamba hiyo ya soka hapa nchini.
Kwa mfano iwapo Mo atakuwa mdhamini wa Simba, anaweza kuweka nembo ya klabu hiyo kama moja ya bidhaa zake kama maji na kujikuta akiwateka mashabiki wote wa klabu hiyo kuyanunua kama itakavyokuwa kwa wale wanaoinyemelea Yanga.
Ni kutokana na hali hiyo, imeelezwa kuwa benki za NMB na NBC nazo zinapiga hesabu kuona ni vipi zinaweza kujitosa kuzidhamini klabu hizo kama sehemu ya kujiimarisha kibiashara.
Alipoulizwa juu ya hali hiyo, Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit, alikiri akisema kuwa huu si wakati wa klabu hizo kulia njaa iwapo zitakuwa makini katika kuingia mikataba na wafanyabiashara au makampuni yanayojitosa kuzidhamini.
Alisema kwamba, kwa upande wa mwenyekiti wao ameonyesha dhamira ya dhati kuikwamua klabu yao kiuchumi na kinachofanyika kwa sasa ni kuandaa mkataba utakaoonekana kuwa na masilahi kwa pande zote mbili.
“Soka kwa sasa linaendeshwa kwa fedha nyingi, bila fedha huwezi kufanya lolote. Tunashukuru kwa upande wetu (Yanga), mwenyekiti wetu ameonyesha nia ya dhati kabisa kuikwamua klabu kiuchumi, nadhani iwapo atafanikiwa, tunaweza kufika mbali sana,” alisema.
Alisema kuwa klabu za Simba na Yanga hazistahili kulia njaa kutokana na utajiri wa mashabiki walionao, kinachotakiwa ni umakini tu katika kuingia mikataba ambayo itakuwa na manufaa kwa pande zote mbili.
Kiongozi huyo alisema wanachama na mashabiki wa Simba na Yanga wasiogope kukaribisha wawekezaji wanaojitokeza kutaka kuzidhamini klabu zao, cha msingi ni kuwa makini katika suala zima la mikataba kuona kama ina manufaa kwao kulingana na hadhi ya klabu zao.
Naye shabiki maarufu wa Yanga, Kais Edwin, alisema: “Ni kweli klabu kama Yanga na Simba zina nafasi kubwa ya kunadi bidhaa au huduma za makampuni na mashirika mbalimbali, kinachotakiwa ni umakini tu kuona ni vipi klabu itanufaika.”
Mmoja wa viongozi wa Simba aliyekataa kutajwa jina kwa kuwa wapo katika mchakato wa kuimilikisha klabu yao, alisema: “Huo ndio ukweli, wafanyabiashara kwa sasa hawana ujanja kwa klabu hizi mbili, kama unataka kuuza bidhaa zako, jitose Simba au Yanga zenye utajiri wa mashabiki. Tunashukuru kwa upande wetu kuna wafanyabiashara wengi na hata mashirika ambayo yameonyesha nia ya kuidhamini Simba na sasa tupo kwenye mchakato wa kukamilisha kila kitu.”
Naye mwanachama maarufu wa Simba, Athuman Mhando, alisema: “Ni kweli kwamba toka utaratibu wa nchi ubadilike katika biashara, wafanyabiashara wamekuwa wakizikimbilia Simba na Yanga wakifahamu zina utajiri wa mashabiki hivyo zitakwenda vizuri kibiashara.
“Utendaji wa rais unatusaidia sana katika hizo klabu kwani makampuni na wafanyabiashara hawawezi kuendelea kutokana na mfumo wa kibiashara wa sasa hapa nchini… naamini wapo wafanyabiashara zaidi watajitokeza kuzikimbilia timu hizi za Simba na Yanga.”
Kutokana na hali hiyo, ni wazi kuwa iwapo viongozi na wanachama wa Simba na Yanga watakuwa makini katika suala zima la kuingia mikataba na yeyote atakayejitokeza kuzidhamini, klabu hizi zinaweza kujikuta zikiwa moto wa kuotea mbali katika soka la Afrika kwani zitakuwa na uwezo wa kusajili wachezaji wa kiwango cha juu, kuwa na nyenzo zote zinazotakiwa katika soka kama viwanja, lakini pia uwezo wa kuajiri makocha na watendaji wengine wenye ubora.
Habari hii imeandaliwa na Michael Maurus, Gray Paul, Regina George na Danieller Kitimbo (TUDARCO), Asma Shemahimbo (RCT) na Ester George.








                                                                                                                                                                                    

Post a Comment

 
Top