WAKATI Yanga kesho Jumapili ikitarajiwa kushuka uwanjani 
kupambana na African Lyon katika mchezo wake wa kwanza 
wa Ligi Kuu Bara msimu huu, jana mwenyekiti wa klabu hiyo,
 Yusuf Manji alifanya kikao kizito cha dakika 270 na wachezaji
 wa kikosi hicho.
Kikao hicho maalum kilifanyika kwenye ofisi za tajiri huyo 
zilizopo jengo Quality Plaza jijini Dar. Kikao hicho kilianza 
saa 2:00 asubuhi hadi saa 6:30 Mchana.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya Yanga zimedai kuwa, 
kikao hicho kilikuwa maalumu  kwa wachezaji pamoja na 
viongozi wa benchi lao la ufundi ambapo walipata kujadili
 mambo mbalimbali yanayowahusu, likiwemo suala la ushiriki wao kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu ambao wanakabiliwa na 
changamoto kubwa ya kutetea ubingwa wao.
“Ni kweli kabisa wachezaji wetu walikuwa na kikao na 
mwenyekiti kwa ajili ya kuzungumza mambo mbalimbali 
yanayowahusu lakini pia ushiriki wao katika michuano ya ligi kuu.
“Kama unavyojua siku chache zilizopita walipatwa na 
hofu kubwa baada ya taarifa kuwa mwenyekiti anataka 
kuachana na timu kutokana na kuchoshwa na matusi ambayo
 amekuwa akikumbana nayo tangu siku aliyotangaza kutaka
 kuikodi timu yetu.
“Kutokana na hali hiyo, pia ametumia mkutano huo kuwaondoa 
hofu hiyo waliyokuwa nayo wachezaji wetu na amewataka 
wapige kazi kwani ushindani msimu huu ni mkubwa na yeye
 yupo nao bega kwa bega kuhakikisha wanawatimizia mahitaji
 yao yote, ikiwa ni pamoja na stahiki zao wanazostahili kupewa
 kulingana na makubaliano yao,” kilisema chanzo hicho cha 
habari na kuongeza:
“Mambo sasa yamekaa sawa, hivyo ile hofu ya kufanya vibaya 
msimu huu ikiwa ni pamoja na mchezo wetu wa kwanza dhidi 
ya African Lyon imeondoka, hivyo Wanayanga tushikamane 
pamoja ili kuhakikisha hatuvurugani tena.”
Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit ili aweze kuzungumzia suala hilo, hakuweza kupatikana kufuatia simu yake ya mkononi kuita tu bila ya kupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe 
wa maandishi hakuweza kujibu.
Hata hivyo, walipoulizwa kuhusiana na suala hilo, baadhi ya 
wachezaji wa timu hiyo ambao waliomba kutotajwa majina yao
 gazetini walisema: “Taarifa hizo ni za kweli kabisa kwani ilikuwa tukutana naye jana (juzi) lakini baadaye tulipewa taarifa kuwa 
amechoka na leo (jana) ndiyo tumekutana naye.”

Post a Comment

 
Top