KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Shiza
Kichuya, ameweka bayana kuwa licha ya kuonyesha uwezo wa hali ya juu katika
mchezo dhidi ya AFC Leopards ya Kenya, Jumatatu ya wiki hii, kwake yeye anaona
bado ana mambo mengi ambayo amedhamiria kuyafanya akiwa na uzi wa Simba.
Kichuya ambaye amejiunga na Simba
hivi karibuni akitokea Mtibwa Sugar, alikuwa moto katika mchezo wa timu hiyo
uliopigwa juzi Jumatatu katika Uwanja wa Taifa, Dar dhidi ya AFC Leopards
ambapo alihusika kwenye mabao matatu ya timu hiyo ya Ibrahim Ajibu na Laudit
Mavugo huku akifunga bao moja.
Kichuya anayemudu kutumia vema mguu
wa kushoto, ameliambia Championi Ijumaa kuwa nia yake tangu alipotua ndani ya timu
hiyo ni kuona anaipa mataji kwa kuonyesha kiwango cha hali ya juu katika kila
mchezo wa timu hiyo.
“Nachokifanya mimi ni kuonyesha uwezo
na kupambana katika kila mchezo wetu kwani nimepania kuipa mataji timu yangu
hii na ili kutekeleza ahadi hiyo, ni lazima niweze kujituma katika kila mchezo
wetu, uwe wa kirafiki au ligi.
“Hapa mbona bado kabisa sijaonyesha
cheche zangu na hata robo bado sijafika, nachotaka kukifanya kwa msimu huu watu
hawataamini, cha msingi wao waendelee kunitazama katika kila mchezo wetu nini
ambacho nitakuwa nakifanya,” alisema Kichuya.


Post a Comment