MSHAMBULIAJI wa Yanga, Mrundi, Amissi Tambwe, amempongeza Mrundi mwenzake wa Simba, Laudit Mavugo kwa kufunga bao lake la kwanza katika michuano ya Ligi Kuu Bara baada ya kujiunga na timu hiyo hivi karibuni.
Juzi Jumamosi, Mavugo aliiongoza Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya Ndanda FC kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Katika mchezo huo Mavugo aliifungia Simba bao la kwanza katika dakika ya 19 akiunganisha mpira uliopigwa na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.
Tambwe alisema kuwa anampongeza Mavugo kwa kufanikiwa kufunga bao katika mechi yake ya kwanza ya ligi kuu, kwani amefanya jambo kubwa ambalo wachezaji wengine hushindwa kufanya katika mechi zao za kwanza.
“Nampongeza kabisa kwani amefanya jambo kubwa kwa sababu kuna wachezaji wengi wa kimataifa hapa nchini ambao wamesajiliwa msimu huu, jana (juzi) wameshindwa kuziongoza timu zao kuibuka na ushindi.
“Lakini yeye amefanikiwa kufanya hivyo ila kwa jinsi nilivyomuona uwanjani, anatakiwa kuongeza bidii, ligi ya Bongo siyo mchezo, bado hayupo makini kuzitumia nafasi anazozipata,” alisema Tambwe ambaye ndiye mfalme wa kuzifumania nyavu katika michuano hiyo ambapo msimu uliopita alifunga mabao 21.


Post a Comment

 
Top