NA EZEKIEL TENDWA
ZIPO sababu nyingi za mashabiki wengi wa soka kupenda kuangalia Ligi Kuu ya nchini England, mojawapo inayotajwa ni kutokana na wenye nchi yao kutumia nguvu nyingi kujitangaza hasa katika vyombo vyao vya habari.
Licha ya kwamba timu za England kwa kipindi cha miaka ya hivi karibuni hazifanyi lolote la maana kwenye michuano ya UEFA na hata ile ya Europa lakini huwabandui kwenye runinga mashabiki wa soka kufuatilia ligi ya nchini humo.
Angalia hata timu yao ya Taifa ilivyotinga nchini Brazil kwenye Kombe la Dunia lililopita. Licha ya kwamba wengi walijua kwamba hawafiki popote lakini kila mmoja alitamani kuwaona jinsi wanavyoshuka na suti zao.
Hawana mpira wa kutisha lakini wana sifa moja kubwa ya kujitangaza. Ni sawa na kikosi cha Ruvu Shooting ambacho ukimsikiliza msemaji wao, Masau Bwire na tambo zake unaweza kusema ni mabingwa wa Afrika kumbe hata nafasi ya nne Ligi Kuu hawawezi kumaliza.
Licha ya ukweli huo lakini kitu cha kipekee kinachoinogesha Ligi Kuu nchini England ni kwamba zipo zaidi ya timu sita ambazo zote zina uwezo wa kupambania ubingwa kitu ambacho huwezi kukikuta Ligi Kuu nchini Hispania.
Pale England hakuna timu ndogo. Ile timu ambayo unaiona kuwa ni ndogo inaweza ikafanya maajabu mfano mzuri ni jinsi Leicester City walivyoushangaza ulimwengu baada ya kutwaa ubingwa msimu uliopita.
Msisimko wa ligi hiyo ndiyo uliowafanya makocha bora duniani kwa sasa kutafuta ulaji hapo. Ukizungumzia makocha wenye majina makubwa huwezi kumwacha Jose Mourinho, Pep Guardiola pamoja na Antonio Conte, wote hao wamehamishia familia zao England.
Leo hii mtu akiambiwa apange timu tatu zitakazogombea ubingwa Ligi Kuu nchini England, jasho litamtoka lakini kwa pale Hispania, La Liga hata kama mtu huyo yupo usingizini atakuambia Barcelona, Real Madrid pamoja na Atletico Madrid.

England utapanga uiache ipi? Wapo Manchester United, Manchester City, Chelsea, Liverpool, Arsenal, Tottenham pamoja na mabingwa watetezi Leicester City. Hapa ndipo penye utofauti mkubwa kati ya Ligi ya England na ligi nyingine.
Ndiyo maana ligi ya Hispania licha ya kwamba wapo wakali kama Barcelona na Real Madrid, wengi hawaifuatilii sana kwani timu hizo ndizo zenye uhakika wa kumaliza nafasi hizo za juu pamoja na Atletico Madrid.
Wakati mashabiki wengi wakihoji nani atamzidi kete mwenzake pale England kati ya Mourinho wa Manchester United, Guardiola wa Man City, Jurgen Klopp wa Liverpool, Conte wa Chelsea, Wenger wa Arsenal, pale Hispania ni Zinedine Zidane na Luis Enrique.
Zidane wa Real Madrid na Enrique wa Barcelona vikosi vyao ndivyo vinavyopewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa achilia mbali kile cha Atletico Madrid kinachonolewa na Diego Simeone ambacho kinajitutumua mara kwa mara kutaka kufuta ufalme wa wawili hao.
Ni nadra kusikia mara kwa mara kwamba Manchester United au Man City imeibuka na ushindi wa mabao zaidi ya 4-0 pale nchini England lakini si ajabu ukisikia Real Madrid au Barcelona wameshinda mabao zaidi ya 5-0 mfululizo.
Mwishoni mwa wiki iliyopita Barcelona walishinda mabao 5-0 na Rela Madrid wakashinda mabao 3-0 ambapo michezo yao ijayo Barcelona anaweza akashinda idadi kubwa zaidi ya hiyo na Real Madrid nao wakapiga mtu zaidi ya hayo kitu ambacho hakitokei mara kwa mara England.
Manchester City walishinda mabao 4-1 dhidi ya Stoke City, lakini mchezo wao ujao dhidi ya West Ham United wanaweza wakapoteza, Manchester United walishinda mabao 2-0 dhidi ya Southampton lakini wanaweza wakaduwazwa na Hull City mchezo ujao. Hiyo ndiyo tofauti kati ya La Liga na EPL.
Bado ligi ya nchini Hispania itaendelea kutawaliwa na timu hizo mbili mpaka pale yatakapofanyika mapinduzi makubwa kwenye soka la nchini humo.

Post a Comment

 
Top