KOCHA Joseph Omog amechukua uamuzi wa kuzungumza na Laudit Mavugo muda mfupi baada ya mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ndanda FC, Jumamosi iliyopita ambapo Simba ilishinda kwa mabao 3-1 lakini Omog hakufurahishwa na aina ya uchezaji wa kucheza kama yuko peke yake uwanjani.

Kocha huyo amemuonya Mavugo kuwa anatakiwa kuhakikisha anawapa pasi wenzake na kucheza kitimu badala ya kuwa mbinafsi.

“Sitaki kuwa na mchezaji mbinafsi, ninataka kuona wachezaji wote wakicheza kitimu kwa washambuliaji kutengenezeana nafasi ya kufunga, mabeki kulinda goli na viungo kuchezesha timu.

“Baada ya mchezo wa Ndanda niliwaita wachezaji wote nikazungumza nao na kuwaambia ninataka umoja na ushirikiano kama timu, sitaki mchezaji akiendelea kucheza na jukwaa kwa lengo la kuwafurahisha mashabiki huku mipango ikiharibika.

“Mfano Mavugo kuna nafasi mbili alipata angeweza kumpa Ajib akafunga na nyingine alipata akashindwa kumpa (Fredric) Blagnon akafunga.

“Jambo zuri ni kuwa Mavugo alinielewa na kukiri kosa ambapo pia aliwaomba msamaha wenzake na kuahidi kubadilika kwenye mechi zijazo,” alisema Omog.

Post a Comment

 
Top