KOCHA wa Simba, Joseph Omog, ameshindwa kuficha hisia zake juu ya winga wa kulia wa timu yake, Shiza Kichuya na kuamua kuanika siri za staa huyo ambazo zinamkuna sana yeye kama mwalimu.

Akimzungumzia Kichuya ambaye amesajiliwa na Simba msimu huu akitokea kwenye klabu ya Mtibwa Sugar, Omog alisema Kichuya ni moja ya wachezaji tegemeo kikosini kwake na anaamini atakuja kufanya makubwa sana siku za usoni.

“Kichuya ni mchezaji mzuri sana zaidi ya watu wanavyomfikiria na baada ya kumuona kwenye mechi hizi chache alizocheza ni dhahiri kuwa ana uwezo wa juu sana na anazunguka uwanja mzima,” alisema Omog.

Kocha huyo alienda mbali zaidi na kutaja mambo yanayomkuna kuhusu ubora wa Kichuya, alisema: “Kichuya ana kasi akitokea pembeni, krosi zake ni za uhakika, anakaba, anafunga na kutoa pasi za mwisho.

“Kwa kifupi Kichuya ni aina ya mchezaji anayeweza kucheza vema na mshambuliaji wa aina yoyote, atawasumbua sana mabeki msimu huu, miguu yake yote miwili inapiga mashuti ya nguvu, naamini kadiri nikiendelea kukaa naye atakuja kuwa mchezaji wa kiwango cha juu sana.”

Kichuya tangu awasili Simba amekuwa akitajwa kama moja kati ya usajili bora zaidi ndani ya klabu hiyo na ndiyo maana ameweza kuingia haraka kwenye mfumo wa Omog.

Post a Comment

 
Top